Amina Omari, Tanga
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella ameiomba serikali kuacha kuagiza kadi za kielektriniki kutoka nje ya nchi na badala yake watumie ambazo zinazalishwa na kiwanda cha hapa nchini ili kujenga uchumi wa viwanda.
Shigella ametoa kauli hiyo alipotembea kiwanda cha kuzalisha vocha na kadi mbalimbali kilichopo jijini Tanga.
Amesema kuwa kwa Afrika viwanda hivyo vipo viwili pekee ambapo kingine kipo nchini Afrika ya Kusini hivyo uwepo wa kiwanda hicho ni mkombozi kwa nchi yetu hasa wakati huu ambapo tupo kwenye mabadiliko ya kiteknolojia.
“Kwa wakati huu ambapo nchi inatumia mfumo wa kieletroniki katika uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, kiwanda hiki kitakuwa mkombozi katika utengenezaji wa kadi badala ya kuagiza nje ya nchi.
Naye Mwekezaji wa kiwanda cha Rushabh Investment, Rashid Liemba amesema kuwa kiwanda hicho kitakuwa ni mkombozi mkubwa kwa nchi za Afrika.
“Kiwanda kilikuwa kianze uzalishaji mapema Machi mwaka huu lakini kutokana na mlipuko wa janga la corona wataalamu wameshindwa kuja kufunga mitambo kwa ajili yakuanza uzalishaji,” amesema Liemba.