Washighton, Marekani
RAIS wa Marekani, Donald Trump ameilaani Korea Kaskazini kwa kitendo cha ukatili kutokana na kifo cha mwanafunzi mmoja wa Marekani, Otto Warmbier.
Trump alisema kifo cha Warmbier kimeimarisha mipango ya utawala wake ya kutaka kuwatetea wengine dhidi ya majanga kama hayo katika mikono ya mataifa yasiyoheshimu sheria.
”Marekani kwa mara nyingine inashutumu ukatili wa utawala wa Korea Kaskazini huku tukimkumbuka mwathiriwa wa hivi karibuni,” alisema Trump.
Mwanafunzi huyo aliachiwa huru baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 15 na alikuwa ameshikiliwa Korea Kaskazini kwa miezi 15. Alifariki dunia siku sita tu baada ya kuachiliwa
Korea Kaskazini ilimrudisha Marekani Warmbier wiki iliopita ikidai kuwa alikuwa hana fahamu kwa mwaka mmoja na kwamba ilikuwa ikimsaidia kibinadamu.
Warmbier ambaye alihukumiwa kwa kujaribu kuiba bango la propaganda kwenye hoteli moja nchini humo, hakuweza kupata fahamu tena.
Familia yake imelaumu kifo hicho katika kile ilichokiita unyanyasaji mkali dhidi ya mtoto wao alipokuwa akishikiliwa na maofisa wa usalama wa Korea Kaskazini.
Akielezea hali ya kijana huyo, alisema alikuwa katika hali ya kutojitambua alipoachiliwa kutoka jela na kuanzia hapo alilazwa hospitalini kwa matibabu.
Madaktari waliokuwa wakimtibu kijana huyo walisema alikuwa na majeraha makubwa ya kuumia mishipa ya fahamu.