26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Rais Samia: NMB wamekuwa nami tangu kuanzishwa Tamasha la Kizimkazi

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amevutiwa na kasi ya Benki ya NMB baada ya kuongeza misaada ya kijamii katika kuadhimisha sherehe za kitamaduni za Kizimkazi visiwani Zanzibar.

Akizungumza wakati wa kilele cha Tamasha la Kizimkazi ambalo awali lilifahamika kama Kizimkazi Day, Rais Samia alisema NMB wamekuwa washirika wazuri tangu kuanzishwa kwa sherehe hizo mwaka 2016, wamekuwa naye bega kwa bega huku wakiongeza misaada kila mwaka.

“Niwashukuru NMB kwa mchango mkubwa wanautoa kwenye sherehe hizi, kila mwaka tunao. Miradi mbalimbali katika sekta ya afya na elimu imefanyika,” alisema Rais Samia.

Alibainisha kuwa tamasha hilo lilipoanza hakujua kama litakuwa kubwa namna hii, ambapo alisema historia yake ilikuwa ni kitendo cha wananchi wa Jimbo la Makunduchi kumfanyia sherehe ya kumuaga baada ya kupitishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu wa urais mwaka 2015.

“Labda niwaambie malengo manne ya tamasha hili; lengo la kwanza ni kuwaleta pamoja wana Kizimkazi, kujuana na kupendana. Pili ni kulinda na kudumisha mila na desturi zetu, tatu kuhamasisha shughuli za maendeleo kupitia utekelezwaji miradi mbalimbalina nne ni kutangaza fursa za kiuchumi zilizopo eneo hili ikiwemo mambo ya kihistoria, fukwe za bahari na utalii wa kiutamaduni,” alisema Rais Samia na kusisitiza kuwa:

“Lilipoanzishwa Tamasha la Kizimkazi mwaka 2016 liliitwa Samia Day, mwaka 2018 likabadilika na kuwa Kizimkazi Day, mwaka huu 2021 linaitwa Tamasha la Kizimkazi, utaona kila mwaka tunabadilika labda litakuja kuwa tamasha la wana Kusini wote,ämesema Rais Samia.

Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Wateja binafsi na Biashara NMB, Filbert Mponzi, akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna alisema benki hiyo imefanya mambo makubwa visiwani Zanzibar hasa kwa kufuata kaulimbiu ya uchumi wa buluu kwa kuwaangalia wakulima wa mwani, wavunaji chumvi na wavuvi.

“Tumetoa mafunzo kwa wakulima wa mwani zaidi ya 3,400 juu ya masuala ya kifedha,pia tumewagusa wavunaji chumvi na wavuvi. Tumefanya haya kwa kuzingatia fursa zilizopo Zanzibar.

“Hadi sasa kwa Zanzibar katika sekta ya elimu na afya tumetumia zaidi ya Shilingi Milioni 257 tangu Agosti mwaka jana (2020), jumla milioni 54 imetolewa kama misaada mwezi huu. Lakini pia katika kuadhimisha sherehe hizi za Tamasha la Kizimkazi kwa mwaka huu tumesaidia vifaa vya hospitali ikiwemo vitanda vya kujifungulia na mabati kwa ajili ya kuezekea baadhi ya shule, ambavyo kwa pamoja vina thamani ya zaidi ya Sh milioni 35,” alisema Mponzi.

Aidha, Mponzi alibainidha kuwa walipewa taarifa kuna Shule ya Msingi Ndijani ambayo aliwahi kusoma Rais Samia, kuna darasa limeangukiwa na mti, hivyo watahakikisha gharama zote za kulikarabati darasa hilo wanazitoa.

Aliweka wazi, NMB ni benki ya wazalendo na inamilikiwa na serikali kwa asilimia 31.8, vilevile imekuwa ikiongoza kwenye vigezo mbalimbali ikiwemo benki yenye mtaji mkubwa, benki yenye uwezo wa kutoa mkopo mkubwa kwa wakati mmoja lakini pia ni benki inayoongoza Tanzania kwa kuwa na huduma bora kwa wateja binafsi.

Vilevile Benki a NMB kwa upande wa Unguja na Pemba ina zaidi ya mawakala 150, mashine za ATM 17 na wamejipanga kuongeza mashine, ambapo pia kuna mashine ya Union Pay Card ambayo inawawezesha watalii kutoa fedha nchini bila usumbufu hali inayowaongezea ari watalii kutembelea Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles