23 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia azitaka taasisi za dini kutoa elimu ya malezi kuondoa mmomonyoko wa maadili

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amezihimiza taasisi za kidini nchini kutoa elimu juu ya malezi bora kama njia ya kukabiliana na mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Rais Samia ametoa wito huo leo, Agosti 31, 2024, katika hafla ya kilele cha mashindano ya kimataifa ya kuhifadhi Quran Tukufu kwa wanawake, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mashindano hayo yalimshuhudia, Amina Yahya kutoka Algeria akitwaa nafasi ya kwanza, huku Nura Mohammad kutoka Marekani akishika nafasi ya pili na Sudeth Said kutoka Jordan akipata nafasi ya tatu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Samia alieleza kuwa ushiriki wa Sheikh Mohammed Abdulkarim Al Issa katika tukio hili ni ishara ya ushirikiano mzuri uliopo kati ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na taasisi mbalimbali za kimataifa. Aliongeza kuwa jambo hili linaonesha kukubalika kwa Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Bin Zubery, katika ngazi za kimataifa.

Dk. Samia pia aliweka wazi kwamba serikali ina imani kuwa BAKWATA na Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania (JUAKITA) zitaimarisha elimu ya dini kwa watoto wa Kitanzania, huku zikibuni mbinu mpya za utoaji wa elimu hiyo ili kuhakikisha maadili mema yanadumishwa katika jamii.

Kwa upande wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Bin Zubery, alieleza kuwa kuna ongezeko la mmomonyoko wa maadili katika jamii, hali iliyompelekea kuandika kitabu kiitwacho ‘Mmomonyoko wa Maadili: Nani Aulizwe?’ Kitabu hiki kinatarajiwa kusaidia jamii ya Watanzania kurejea kwenye maadili mema.

Mufti na Sheikh Mkuu pia aliishukuru serikali, kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, na wadau wengine kwa kuwezesha kufanikisha mashindano hayo. Aliongeza kuwa, matarajio yake ni kwamba Watanzania watakuwa wamejifunza maadili mema yaliyosisitizwa na Mwenyezi Mungu kupitia mashindano hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles