23.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia kuhudhuria Mkutano wa Tisa wa Wakuu wa Nchi na Serikali China na Afrika

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa tisa wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) utakaofanyika jijini Beijing, China, kuanzia Septemba 4 hadi 6 mwaka huu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, alisema kuwa Rais Dk. Samia atahudhuria mkutano huo kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping. Balozi Kombo alibainisha kuwa mikutano ya FOCAC hufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa kubadilishana kati ya China na nchi moja ya Afrika.

“Jukwaa la FOCAC lilianzishwa mwaka 2000 na Jamhuri ya Watu wa China kwa lengo la kukuza ushirikiano na maendeleo ya pamoja kati ya China na Afrika. Tangu kuanzishwa kwake, mikutano ya kilele nane ya Wakuu wa Nchi na Serikali imekwisha kufanyika,” alisema Balozi Kombo.

Rais Dk. Samia ataongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo, akiungana na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nchi zaidi ya 40 kati ya 54 za Bara la Afrika. Mkutano huo pia utahudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat.

Kwa mujibu wa Balozi Kombo, Serikali ya China imemteua Rais Dk. Samia kuhutubia katika hafla ya ufunguzi wa mkutano huo, itakayofanyika Septemba 5, ambapo atawakilisha Kanda ya Afrika Mashariki. Mkutano huo utaongozwa na kaulimbiu isemayo “Kushirikiana ili Kuendeleza Usasa na Kujenga Jamii Bora ya China na Afrika kwa Mustakabali wa Pamoja.” Lengo ni kuhamasisha viongozi wa Afrika na China kujadili masuala muhimu ya kuimarisha ushirikiano na kuongeza kasi ya maendeleo kwa pande zote mbili.

Mkutano wa FOCAC utagawanyika katika mikutano minne ya ngazi ya juu itakayofanyika kwa wakati mmoja, ambapo kila nchi inapaswa kuchagua mada moja ya kujadili. Tanzania itajikita katika mada ya maendeleo ya viwanda na kilimo cha kisasa, mada iliyozingatia Mpango wa Maendeleo wa Tatu wa Miaka Mitano, ambao ni sehemu ya mwisho wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2025.

Balozi Kombo aliongeza kuwa, akiwa nchini China, Rais Dk. Samia atafanya mkutano wa pande mbili na Rais Xi Jinping, ambapo watajadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya nchi hizo. Baada ya mazungumzo hayo, watashiriki katika hafla ya kutia saini Hati za Makubaliano kuhusu kuifufua Reli ya TAZARA.

Rais Dk. Samia pia atafanya mikutano ya pembezoni mwa mkutano wa FOCAC, ikilenga kukuza uhusiano wa kidiplomasia na kuvutia wawekezaji wa China kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali. Pia, atakutana na Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Watu wa China kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya Bunge la Tanzania, Baraza la Wawakilishi, na Bunge la China.

Mbali na hayo, Rais Dk. Samia atafanya mazungumzo na kampuni za China ambazo zina nia ya kufanya uwekezaji mkubwa na kufungua ofisi zao nchini. Pia atakutana na wawakilishi wa kampuni kubwa za China katika hafla ya chakula cha jioni yenye lengo la kuhamasisha uwekezaji nchini Tanzania.

Kwa upande mwingine, Tanzania inatarajia kuwasilisha miradi mbalimbali kwa ajili ya kufadhiliwa chini ya mpango kazi wa mwaka 2025-2027, ikiwemo ujenzi wa mtandao wa mawasiliano vijijini awamu ya pili, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 400 awamu ya pili na tatu, ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi (VETA) awamu ya pili, na ujenzi wa barabara za Zanzibar zenye urefu wa kilomita 277.7.

Mkutano wa FOCAC una malengo makuu matatu: kuendelea kudumisha ushirikiano kati ya Tanzania na China, kujadiliana na kukubaliana namna ya kuongeza ushirikiano katika maeneo ya kipaumbele kwa maendeleo ya Taifa, na kuibua fursa mpya za ushirikiano kwa manufaa ya pande zote mbili. Pia, Serikali ya Awamu ya Sita inatarajia kutumia mkutano huo kutangaza maboresho yaliyofanywa katika sera na sheria za biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka China.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles