Na Mwadishi Wetu, Mtanzania Digital
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa vyama vya siasa kujipanga kikamilifu kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa, akisisitiza umuhimu wa kutumia muda huu kuwafikia wapiga kura badala ya kusubiri matokeo na kulalamika.
Akihutubia leo Oktoba 11, 2024 Chamwino mkoani Dodoma baada ya kushiriki katika zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura, Rais Samia amewataka viongozi wa vyama vya upinzani, hususan Chadema, kuelekeza juhudi zao katika kushawishi wananchi na kuwapa imani ya uongozi wao.
Amesema vyama vya upinzani vinatumia muda mwingi katika kutoa malalamiko kuhusu mchakato wa uchaguzi badala ya kutoa hoja na sera zinazoweza kuwavutia wapiga kura.
“Kujipanga vizuri na kufikia wananchi kwa sera madhubuti ni njia bora ya kujenga imani na kuwa na nafasi bora kwenye uchaguzi. Hakuna uchaguzi usio na changamoto, lakini malalamiko yasiyokoma yanaweza kupunguza ari ya wapiga kura na kuvunja imani ya wananchi kwa vyama vya siasa,” alisema Rais Samia.
Kwa muda mrefu, vyama vya upinzani nchini, vimekuwa vikihoji uhalali wa mchakato wa uchaguzi, hali ambayo mara nyingi imetafsiriwa kuwa kikwazo kwa wao kujionyesha kama mbadala wa kuaminika kwa wananchi.
Rais Samia alisisitiza kuwa, ili kuboresha demokrasia nchini, ni muhimu kwa vyama vya siasa, hasa vya upinzani, kujikita katika hoja za msingi, kujenga mikakati yenye kuleta mabadiliko, na kuonesha uwezo wao wa kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Kwa kumalizia, Rais Samia aliwaasa viongozi wa vyama vya siasa kuepuka malalamiko yasiyokoma na badala yake kujielekeza kwenye kujenga hoja na sera zinazoonyesha dhamira yao ya kweli ya kuleta maendeleo na mabadiliko nchini.