32.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 12, 2024

Contact us: [email protected]

Mchungaji Tengwa awataka Watanzania kuliombea Taifa

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Mchungaji wa Kanisa la Uamsho na Matengenezo ya Kiroho Ulimwenguni, Mwalimu Augustine Tengwa, amewataka Watanzania kuendelea kuliombea Taifa lao kwa ajili ya amani, upendo, na usalama.

Amesema kwa kuzingatia umuhimu wa uchaguzi wa mwaka huu na mwaka 2025, ni muhimu kwa kila raia kujitolea kuliombea taifa na kulinda uzalendo wao.

Akizungumza leo Oktoba 11, 2024, jijini Dar es Salaam akiwa na wachungaji wengine, Mchungaji Tengwa alisisitiza juu ya umuhimu wa amani na kuwataka Watanzania wote kushikamana na kumwombea Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wengine wa serikali.

Alieleza kuwa jukumu la kusimamia amani linaanzia kwa wananchi, lakini pia aliwahimiza vyombo vya ulinzi na usalama kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu ili kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unadumishwa.

“Nimepewa maono na Mungu kuwataka Watanzania kuitunza amani. Hivyo ninawaomba nyinyi kama waandishi wa habari mfikishe ujumbe huu kwa kila Mtanzania, na pia ninatoa rai kuliombea taifa la Tanzania hasa wakati huu tunapoelekea kwenye uchaguzi,” alisema Mchungaji Tengwa.

Nabii Alpha Kiamba, ambaye alihudhuria mkutano huo, alitoa wito kwa Watanzania kupuuza taarifa zenye lengo la kuwagawa, akisisitiza kuwa upinzani nchini unapaswa kufanywa kwa hekima na si uadui. Alisema kuwa ni muhimu kwa wananchi kushikamana kwa sala na maombi ili kuhakikisha usalama wa taifa na mshikamano wa kitaifa.

“Suala la upinzani nchini lifanyike katika hekima za Mungu na sio uadui, ndiyo maana tunahitaji watu kuombea Taifa. Kila mkoa waingie kwenye maombi kuombea nchi pamoja na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine,” alisema Nabii Alpha.

Akiendelea, Nabii Alpha alieleza kuwa wao kama watumishi wa Mungu wamekuwa mabalozi wa amani na mara kwa mara wanafanya maombi kwa ajili ya taifa. “Tunaamini Tanzania bila maombi hakuna Taifa,” alisema, akisisitiza kuwa maombi yanayofanywa na viongozi wa dini ni muhimu katika kuimarisha umoja na amani nchini.

Wito huu wa viongozi wa dini ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuhamasisha wananchi kushiriki katika kuimarisha amani na utulivu, wakati Tanzania ikielekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles