26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, November 21, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia ataka mpango madhubuti kuleta maendeleo Afrika

*Asema maisha bora yako Afrika

*Benki ya Dunia yasema bado kuna kazi ya kufanya hasa kwenye elimu

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan amesema suala la maendeleo ya rasilimali watu barani Afrika haliwezi kuja kwa kubahatisha badala yake lazima kuwe na mpango madhubuti ambao utatekelezwa kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake.

Sehemu ya viongozi wanaoshiriki mkutano huo.

Dk. Samia ameyasema hayo leo Julai 26, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa Wakuu wa Nchi Barani Afrika unaojadili Mtaji wa Rasilimali watu hususan vijana.

Amewasihi viongozi hao kuwa hakuna muda mwingine sahihi wa kujadili mambo muhimu zaidi ya mkutano huo uliopo kwa mustakabali wa Afrika.

Dk. Samia amesema ni muhimu kwa nchi za Afrika kuendeleza vijana kufikia ndoto zao ili kukuza rasilimali watu kwa maendeleo ya uchumi kwa nchi.

“Suala la maendeleo ya mtaji wa rasilimali watu Afrika haliwezi kuja kwa kubahatisha na haina mbadala lazima tuwe na mpango madhubuti ya kuhakikisha rasilimali watu Bara la Afrika inaendelezwa kwa manufaa ya bara hili kwa maendeleo yetu.

“Afrika ina idadi kubwa ya vijana, hivyo ni fursa ya pekee katika mageuzi ya uchumi katika bara letu kuliko kuwaacha vijana hawa kwenda kutafuta fursa Ulaya na kupata tabu njiani, tuwawezeshe kwani maisha bora yapo Afrika,” amesema Dk. Samia.

Amesema katika kuhakikisha Taifa la Tanzania linalinda na kutunza rasilimali watu nchi imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kutenga fedha kwenye Afua za lishe na kulinda afya ya mama na mtoto.

Dk. Samia amesema kuweka msingi bora wa elimu kuanzia mtoto kwa kumpatia lishe bora na kuanzisha vituo vya vya elimu ya awali ni jambo la muhimu katika ustawi wa jamii yetu.

“Kutokana na kuwepo na mimba za utotoni ili kuepuka hili lazima tuwafundishe watoto uzazi wa mpango kwa sababu ongezeko la watu Afrika linakua sana,” amesema Dk. Samia.

Amesema moja ya mikakati ambayo imeanzishwa na Serikali katika kusaidi wananchi ni pamoja na uanzishwaji wa mfuko wa kupunguza umaskini TASAF lakini pia mfuko wa kusaidia vijana kiuchumi pamoja na kuwarudisha wanafunzi waliopata ujauzito wakiwa shuleni baada ya kujifungua.

Aidha, amesema kufikia ajenda ya Mwaka 2063 kuna malengo mengi ambapo ameyataja baadhi kuwa ni Afrika kuwa na mafanikio jumuishi, kuzingatia misingi ya utawala bora, demokrasia na haki za binadamu na kwamba hali itakuwa nzuri iwapo nchi za Afrika zitakubali kuwekeza katika rasilimali watu.

“Kuongeza uwekezaji katika sekta nyingine kama afya, elimu, miundombinu na kufungua fursa katika rasilimali watu ni wajibu wetu, kuunganisha serikali na asasi za kiraia kwaajili ya rasilimali watu,” amesema Dk. Samia.

Amesema uwekezaji wa rasilimali watu ni wajibu wa kimaadili ili kujenga Afrika yenye uchumi wezeshi kwa kuwawezesha vijana kufikia ndoto zao.

Naye Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Dk. Victoria Kwakwa amesema Afrika inakabiliwa na changamoto katika masuala ya rasilimali watu mkutano huo ni muhimu kwani unatoa fursa ya kujadili namna ya kuondoa changamoto.

Akizungumzia kuhusu elimu amesema Afrika inachangamoto kubwa ya elimu kwani asilimia 80 ya watoto wa Kusini mwa Jangwa la Sahara hawajui kusoma wala kuandika, maboresho katika sekta ya elimu yatasaidia kukuza mtaji wa rasilimali watu katika nchi za Afrika.

“Uganda imekuwa ya kwanza kuondoa udumavu kwenye maendeleo endelevu na Kenya imeboresha kwa asilimia 50 katika sekta ya elimu,” amesema Dk. Kwakwa

Aidha, Dk. Kwakwa ameipongeza Tanzania kwa kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kwa kuwarudisha shuleni wanafunzi waliopata ujauzito baada ya kujifungua.

Sambamba na hayo amesema kuwa zaidi ya asilimia 50 ya walimu hawafundishi vizuri hivyo kuna haja ya kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya walimu ili kufikia maendeleo na kuboresha sekta ya rasilimali watu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles