27 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia ataka majibu zaidi saratani ya mlango wa kizazi, matiti Kanda ya Ziwa

Na Clara Matimo, Mwanza

Baada ya kuendelea kuwepo na kuongezeka wagonjwa wa Saratani Mikoa ya Kanda ya Ziwa, huku sababu ikitajwa kuwa ni uchafuzi wa mazingira kutokana na uchenjuaji dhahabu, Rais Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando (BMC) kufanya utafiti utakaoleta majibu zaidi ya hayo.

Rais Samia amesema endapo ugonjwa wa saratani ungekuwa unasababishwa na zebaki kutokana na uchafuzi wa mazingira katika vyanzo vya maji yanayotoka kwenye migodi ya madini kama ambavyo watafiti wamebaini, basi tatizo hilo lingewakumba wanawake na wanaume lakini tafiti zinaonyesha waathirika zaidi ni wanawake ambao hupata saratani ya mlango wa kizazi na matiti.

Rais Samia Suluhu Hassan, akikata utepe katika chumba chenye mashine ya MRI BMC, kuashiria uzinduzi wa kuanza kutumika kwa mashine hiyo iliyonunuliwa na serikali kwa gharama ya Sh bilioni 2.4 kupitia mradi wa ushirika na Serikali ya Uholanzi, kushoto ni Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Doroth Gwajima, kutoka (kulia) ni Mwenyekiti wa Bodi ya BMC ambaye ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Renatus Nkwande, akifuatiwa na Rais wa TEC Askofu Gervas Nyaisonga. Picha na Clara Matimo.

Kiongozi huyo wa nchi ametoa agizo hilo leo Alhamisi Novemba 18, jijini Mwanza wakati akihutubia katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya BMC baada ya kuzindua huduma ya mashine mpya  ijulikanayo kama Magnetic Resonant Imaging(MRI) iliyogharimu Sh bilioni 2.4 kupitia mradi wa ushirika na Serikali ya Uholanzi pamoja na mnara wa kumbukumbu ya miaka 50 ya BMC iliyofunguliwa na kuanza kutoa huduma mwaka 1971 na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

“Tafiti zijikite zaidi kubaini chanzo cha saratani hizo na kwa nini mikoa ya kanda ya ziwa inaongoza kwa waathirika wa saratani ambapo wanawake ndiyo wahanga wakubwa ambao hukubwa na saratani ya shingo ya  kizazi na matiti.

“Kuna sababu kadhaa zinatolewa wengine wakidai ni uchafuzi wa mazingira kutokana na uchimbaji wa madini na kutumia zebaki ambao watu wanafanya  uchenjuaji wa madini kwenye mito  ambapo maji hayo watu huyatumia kwa kunywa  hivyo kusababisha kuenea kwa saratani.

“Lakini idadi kubwa inaonyesha ni wanawake na ni saratani za shingo ya  kizazi na matiti, hapa ndipo panapoleta swali kwa nini? Kama ni zebaki ingekuwa kwa wote wanawake na wanaume lakini idadi kubwa ni wanawake na ni saratani za matiti na shingo ya kizazi hivyo fanyeni  utafiti mbaini ni kwa nini  ili tuweze kuchukua hatua  na tupunguze kwa kiasi kikubwa balaa hili linalotuzonga,”ameagiza Rais Samia.

Amesema inasikitisha kuona idadi ya wagonjwa wa saratani inaongezeka kwa kasi kutoka wagonjwa 1,200 mwaka 2019 hadi kufikia wagonjwa 1,500 mwaka 2021 hali inayokwamisha uzalishaji mali na kufifisha jitihada za serikali katika kuleta maendeleo. 

Amesema serikali kwa kushirikiana na Kanisa Katoliki imeboresha huduma za afya hospitalini hapo kwa kuongeza vitanda kutoka 550 hadi 950, kila mwaka  inatoa Sh bilioni 20 kwaajili ya kulipa mishahara watumishi 1,161 pamoja na ruzuku ya dawa kwa wastani wa Sh bilioni moja, zaidi ya Sh milioni 200 kwa ajili ya uendeshaji wa hospitali, ambapo amefafanua kwamba hivi karibuni imetoa Sh Bilioni 4.2 kwa ajili ya kuboresha huduma za kibingwa,ununuzi wa vifaa tiba, huduma za dharula na wagonjwa mahututi, ikiwa ni moja ya mkakati katika kuboresha Sekta ya Afya nchini

“Wito wangu kwenu wataalamu wa vifaa tiba ikiwemo mashine ya MRI ambayo nimeizindua leo vitunzeni ili vidumu na kutoa huduma muda mrefu  maana fedha zilizotumika kununua mashine hiyo tumechukua mkopo ili turahisishe huduma za afya, tutazilipa sisi wenyewe watanzania kupitia kodi zetu, uwepo wa mashine hii utaokoa Sh bilioni 1.9 ambazo serikali ingezitumia kwa mwaka mmoja kwa ajili ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi kupata matibabu,”alieleza Rais Samia.

Pia amemuagiza Waziri wa Afya, Dk. Dorothy Gwajima, kusimamia fedha zilizotolewa na serikali kuboresha miradi mbalimbali  ya afya huku akiahidi kuendelea kutoa ajira za watumishi kadiri inavyowezekana ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa wafanyakazi hospitalini hapo.

Aidha, Rais Samia  Suluhu Hassan aliipongeza BMC na Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki cha Sayansi ya Afya na Tiba Bugando (CUHAS) kwa kufanya utafiti na kugundua kimelea kipya ambacho kilikuwa hakijawahi kugunduliwa duniani kijulikanacho kwa jina la Enterobacter bugandesis na matibabu yake hugharimu Sh milioni 4.5.

Kwa mujibu wa Naibu Makamu Mkuu Taaluma na Utafiti, CUHAS, Profesa Stephen Mshana, Kimelea hicho ni sugu na hakitibiwi na dawa za kawaida lakini huwapata watoto wachanga walio na umri chini ya mwezi mmoja na wanaozaliwa kabla ya kutimiza muda(njiti) au waliopata maambukizi (Neonatal Sepsis) dalili zake ni kupata homa kali, degedege, kushindwa kunyonya na kutokukua vizuri.

Awali, akimkaribisha Rais Samia katika maadhimisho hayo, Dk. Gwajima, aliwasisitiza wananchi wa mikoa ya kanda ya Ziwa kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya UVIKO-19 ili wajikinge na maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya korona pamoja na kujiunga na bima ya afya ili wawe na uhakika  wa kupata matibabu watakapo ugua.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa  BMC, Dk. Fabian Massaga, amesema kupatikana kwa kipimo hicho  cha MRI kitakuwa ni faraja kwa wakazi wa Mikoa ya  Kanda ya Ziwa kwa kuwa kinahitajika zaidi katika magonjwa ya ubongo na mifupa maana  kinauwezo wa kuona ugonjwa mdogo katika hatua za mwanzo.

Amesema BMC tangu ianzishwe imeendelea kutoa huduma za Tiba mafunzo na tafiti kwa watanzania wote bila kubagu kabila, dini, rangi au itikadi ya kisiasa ya mtu yeyote.

“Tunaendelea kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa wagonjwa kutoka mikoa nane ya kanda ya ziwa ambayo ni Mwanza, Geita, Simiyu, Tabora kigoma, Mara, Shinyanga, Kagera yenye takribani wakazi milioni 18 kauli mbiu ya maadhimisho haya inasema Bugando mpya yenye huruma na upendo,”amesema Dk. Massaga. 

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya BMC ambaye ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Renatus Nkwande, amesema  wanakabiliwa na upungufu  wa wafanyakazi kwani waliopo ni 1800  lakini wanaohitajika ni 2,554.

BMC inamilikiwa na Serikali pamoja na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) ambapo leo maadhimisho hayo yalitanguliwa na adhimisho la Ekaristi Takatifu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles