MOSCOW, URUSI
RAIS Vladimir Putin wa Urusi, amesema taifa lake limewatambua watu wawili wanaotuhumiwa kumwekea sumu kachero wa zamani wa Urusi nchini Uingereza, lakini amepuuza madai kuwa walikuwa sehemu ya majasusi wake.
Akizungumza katika mkutano wa jukwaa la uchumi humo Vladivostok, kiongozi huyo wa Urusi alisema watu hao waliotuhumiwa kumshambulia kachero huyo aliyeisaliti Urusi kwa Uingereza, Sergei Skripal na binti yake Yulia ni raia wa kawaida na hakuna taarifa yoyote ya kuwahusisha na uhalifu, ingawa alishindwa kueleza walichofuata Uingereza.
Polisi wa Uingereza waliwatambua wawili hao kama Alexander Petrov na Ruslan Boshirov na walidai walikuwa sehemu ya mtandao wa kiusalama wa Urusi (GRU).
Lakini Putin alisema: “Tumechunguza watu hawa kuangalia utambulisho wao. Tumewabaini ni kina nani.
“Tuna matumaini watajitokeza karibuni na kutuambia kila kitu wenyewe. Itakuwa vyema kwetu sote. Hakuna kitu jinai katika hili’.
Kauli hii ya Putin imekuja siku chache baada ya Urusi kuonyesha misuli yake ya kijeshi kwa kufanya mazoezi makubwa yaliyoambatana na uonyeshaji makombora yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia.
Tukio hilo lilishirikisha askari zaidi ya 300,000 wakiwamo 3,000 wa China katika hatua iliyokera magharibi.
Washukiwa hao wawili walinaswa na CCTV katika kituo cha treni cha Salisbury, muda mfupi baada ya saa 10 jioni ya Machi 3, mwaka huu, siku ambayo Skripal aliwekewa sumu.
Uingereza ilidai washukiwa hao walizuru Uingereza mara kadhaa wakijifanya matajiri wa Urusi ili ziara yao ya Machi, mwaka huu isishtukiwe.