33.9 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Magufuli kuzindua mradi mkubwa wa maji Tabora

Na Allan Vicent, Tabora

Rais Dk. John Magufuli anatarajia kufanya ziara ya siku moja mkoani Tabora Januari 30, mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine atafungua mradi mkubwa wa maji kutoka ziwa Victoria kuja mkoani humo uliogharimu kiasi cha Sh bilioni 617.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Philemon Sengati amesema wakazi wa Mkoa huo wanamsubiri kwa hamu kubwa kutokana na mambo makubwa aliyowafanyia katika kipindi kifupi.

Amesema rais ameupa heshima kubwa Mkoa huo kwani katika kipindi cha miaka mitano tu (2015-2020) ameweza kutekeleza miradi mingi na mikubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo maji, afya, elimu, miundombinu ya barabara na mingineyo ambayo imebadilisha mandhari ya mkoa huo.

Amebainisha kuwa, Tabora sasa inang’aa na kumelemeta kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya utawala wa Rais Magufuli, hivyo wananchi wana shauku na hamu kubwa sana kumwona.

Dk. Sengati amefafanua kuwa akiwa mkoani humo rais atafungua rasmi mradi huo wa maji kutoka ziwa Victoria uliogharimu kiasi cha sh bil 617 ambao unatarajiwa kunufaisha wakazi zaidi ya Sh milioni 1.2 vikiwemo vijiji 148, tukio hilo litafanyika katika eneo la tenki la maji la Kaze Hill.

Ametaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa Jengo la Wagonjwa wa dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo, Kitete, ambalo litawekewa jiwe la msingi kabla ya kuhutubia wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika uwanja wa mpira wa miguu wa Ali Hassan Mwinyi.

“Kwa mkoa wetu jumla ya kiasi cha fedha kilichotolewa na serikali katika kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ni pamoja na Sh bilioni 30 za ujenzi wa hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati na Sh bililioni 159.8 kwa ajili ya kugharamia miradi ya umeme ya TANESCO na REA.

“Kiasi kingine ni Sh bilioni 42 za elimu bila malipo zilizotolewa kwa ajili ya shule za msingi na sekondari huku kiasi cha Sh bilioni 39.6 kikitolewa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule zote.

“Kiasi kingine ni Sh bilioni 617 zilizotolewa kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji ya ziwa Victoria ambao ataufungua atakapowasili na Sh bilioni 20.9 za ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya maji,” amesema.

Aidha katika utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi aliongeza kuwa serikali ilitoa kiasi cha Sh bilioni 481.6 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za kiwango cha lami na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Tabora.

Ametoa wito kwa wakazi wote wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kuanzia saa 1 asubuhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles