MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli, amemwapisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango atakayeshughulikia Sera, Adolf Ndunguru na Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Msafiri Mbibo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao ilifanyika jana na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji.
Wengine ni makatibu wakuu, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Akizungumza baada ya kuwaapisha, Rais Magufuli ameitaka TRA na Wizara ya Fedha na Mipango kupanua wigo wa kodi kwa kuongeza idadi ya walipa kodi na kuibua vyanzo vipya vya mapato, pamoja na kujenga mazingira rafiki kwa watu wengi zaidi kulipa kodi ili kuongeza makusanyo ya kodi.
Pamoja na hali hiyo Rais Magufuli, alieleza kutoridhishwa na utendaji kazi wa TRA ambayo mpaka sasa inakusanya kodi kwa walipa kodi milioni 2.7 tu kati ya Watanzania wote zaidi ya milioni 55.
Kutokana na hatua hiyo mkuu huyo wa nchi alisema kwa mtindo huo TRA itakuwa inazidi kuwakamua walipa kodi wachache wakati ingeweza kupanua wigo wa kodi na kuweka viwango vya kodi vinavyolipika na vitakavyowavutia watu wengi zaidi kulipa kodi.
“Ukienda mipakani wafanyabiashara wanafungua maduka upande nchi za wenzetu na sio upande wa Tanzania, na sababu ni kwamba wakifungua upande wa Tanzania wanasumbuliwa na TRA, wekeni viwango vya kodi vinavyolipika ili watu wengi waweze kulipa kodi badala ya kukwepa,” alisema Rais Magufuli.
Licha ya hali hiyo alieleza kutofurahishwa na mrundikano wa kesi za kodi mahakamani na ametaka tatizo hilo lifanyiwe kazi kwa kuwa linasababisha kodi nyingi kutolipwa kwa kusubiri mivutano ya kesi.
Hata hivyo alimpongeza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji kwa ufuatiliaji mzuri wa fedha za bajeti zinazoelekezwa katika miradi mbalimbali na kuchukua hatua zinazostahili ikiwemo kuzirejesha hazina na kuzielekeza mahali pengine zinapohitajika.
Aidha, aliwataka Ndunguru na Mbibo kwenda kurekebisha dosari zote zilizopo katika ofisi zao ikiwa ni pamoja na kuwaondoa watumishi wanaoonekana kuwa kikwazo cha kutekeleza mipango ya Serikali.
Kwa upande wake Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, alisema viongozi hao wanatarajiwa kufanya vizuri zaidi katika nafasi walizopewa hivi sasa hasa ikizingatiwa kuwa wanakwenda kufanya kazi katika ofisi zenye mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.
Naye Dk. Ashatu Kijaji na Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere walimshukuru Rais Magufuli kwa uteuzi wa viongozi hao na wameahidi kwenda kusimamia kwa ukaribu zaidi utekelezaji wa fedha za bajeti na kufanyia kazi changamoto ya kupanua uwigo wa kodi na kuongeza idadi ya walipa kodi.
AMPA POLE MCHUNGAJI MSIGWA
Wakati huo huo, Rais Magufuli pamoja na mkewe Janeth wametoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu na kutoa mkono wa pole kwa familia ya Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa, ambaye amefiwa na dada yake Tryphosa Simon Sanga aliyefariki dunia Machi 30, mwaka huu kwa ajali ya gari jijini Dar es Salaam.
Wakiwa nyumbani kwa marehemu Kimara Stopover, Rais Magufuli na mkewe waliungana na wanafamilia kumwombea marehemu apumzike mahali pema peponi.