29.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Zitto: Tumewasilisha majibu hoja zote za msajili

PATRICIA KIMELEMETA – dar es salaam

KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema wamejibu hoja zote za Msajili wa Vyama vya Siasa, ambaye aliwapa siku 14 waeleze kwanini chama chao kisifutiwe usajili wa kudumu.

Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini, alisema hayo jana wakati akiwahutubia wajumbe wa jimbo hilo wa ngazi ya matawi na kata.

Alisema majibu ya hoja hizo za msajili waliyawasilisha jana.

“Leo (jana) tumewasilisha maelezo yetu kwa Msajili wa Vyama ya Siasa, lakini pia nimeona ni muhimu sana kukutana nanyi ili muelewe maana ya tishio hili la Serikali kutaka kukifuta chama chetu,” alisema Zitto. 

Alisema yeye ni mwakilishi wao kupitia chama hicho ambacho pia kimetoa Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji na madiwani 19 kati ya 26 wa jimbo hilo.

Zitto alisema ACT ikifutwa watakosa mbunge na kuvunjika kwa Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Alisema jambo hilo lina maana kuwa watu wa Kigoma Mjini na Mkoa wa Kigoma watakosa mbunge wa kupaza sauti na kuwatetea bungeni.

Zitto alisema pia watakosa mbunge wa kwenda kuhimiza kumalizwa kwa mradi wa maji uliocheleweshwa tokea mwaka 2015.

 “Mtakosa mbunge wa kupaza sauti juu ya uonevu wa watu wa Uhamiaji dhidi yenu, mtakosa mpaza sauti juu ya utaifishwaji wa nyavu za wavuvi wetu kwenye Ziwa Tanganyika, ”alisema.

Zitto alisema Kigoma imeachwa nyuma mno, imebaki kuwa mkoa pekee usiounganishwa na mtandao wa barabara na mikoa mingine.

Alisema wakiwa kwenye eneo muhimu la kijiografia linalopakana na nchi mbili za Burundi na DRC Congo, lakini taratibu za uendeshaji uchumi na miundombinu linawazuia kunufaika na ujirani huo. 

Zitto alisema alitumia miaka minne ya kuwa mwakilishi wao na kushauri njia nzuri ya kuwatoa hapo walipo.

Alisema watapigania upanuzi na uboreshaji wa bandari ya Kigoma ili kulikamata soko la Zambia na DRC ambalo linatumia asilimia 70 ya mizigo yote ya Bandari ya Dar es Salaam. 

Hata hivyo, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alipoulizwa kuhusu kupokea barua ya Zitto, alijibu kuwa yupo Dodoma katika mkutano.

“Tupo Dodoma kwenye kikao, hivyo basi siwezi kulizungumzia suala hilo kwa muda huu,” alisema Nyahoza.

Wiki iliyopita, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilimwandikia Zitto barua ya kutishia kuifuta ACT kwa madai ya kutowasilisha hesabu za ukaguzi za 2013/14, hivyo kutokidhi matakwa ya barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, hatua inayokiuka sheria ya vyama vya siasa sura ya 258.

Tuhuma nyingine katika barua hiyo ya msajili yenye kumbukumbu namba HA.322/362/20/98 ya Machi 25 kwenda ACT-Wazalendo, ni vitendo vya uvunjifu wa sheria ikiwamo kuchoma moto bendera za Chama cha CUF baada ya mahakama kutoa hukumu katika kesi namba 23 ya 2016.

Barua hiyo ilieleza kuwa vitendo hivyo vinafanywa na mashabiki wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ambao wanadaiwa sasa ni wanachama wa ACT-Wazalendo, ambavyo ni kukiuka kifungu cha 11C cha sheria ya vyama vya siasa.

Tuhuma nyingine ni chama hicho kutumia dini katika siasa zake baada ya wanaodaiwa kuwa mashabiki wake kuonekana katika mitandao wakipandisha bendera ya ACT-Wazalendo kwa kutumia tamko la dini ya Kiislamu (Takbir), kitendo kinachokiuka kifungu cha 9 (1)(C) cha sheria hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,905FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles