27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

AMUNIKE AANIKA VIGEZO KUITWA STARS

*Amfagilia Fei Toto, asema akiongezewa mavitu hata Barcelona anakimbiza


JENNIFER ULLEMBO-DAR ES SALAAM

KOCHA mkuu wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Emmanuel Amunike, amesema si kila mchezaji anayecheza Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), anastahili kukichezea kikosi hicho.


Amunike alitoa kauli hiyo jana alipotembelea Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Bingwa, Rai na Dimba.
Alisema kikosi cha timu ya taifa kinahitaji wachezaji wapambanaji, ambao wapo tayari kulipigania taifa lao kwa ajili ya kusaka ushindi.

Alisema kamwe hawezi kutoa nafasi kwa wachezaji ambao wamekuwa wakionyesha kiwango kinachobadilika badilika, kwa vile hawatakuwa na msaada kwa timu ya taifa.


“Najua kuna mashabiki ambao wanapenda kumwona mchezaji fulani akiitwa lakini mimi ni kocha mwenye taaluma, sifanyi jambo kwa kumfurahisha mtu.


“Stars itajengwa na wachezaji wanaopambana, kambi yetu huchukua siku chache, sasa mchezaji akishindwa kudumisha kiwango kizuri kwenye mechi za ligi itakuwaje huku.


“Mchezaji anaonyesha kiwango kizuri kwenye mechi moja ya ligi, baada ya hapo anapotea kabisa, sasa huyo utampaje nafasi katika kikosi kinachosaka ushindi,” alihoji Amunike.


Amunike ambaye ni staa wa zamani wa Barcelona na timu ya Taifa ya Nigeria ‘Super Eagles’, hakusita kuwamwagia sifa viungo, Feisal Salum ‘Fei Toto’, anayeichezea Yanga na Mudathir Yahya, wa Azam akisema ni wachezaji anaojivunia ubora wao katika kikosi cha Taifa Stars na kuongeza kuwa ni hazina kwa taifa.


“Feisal anaweza kucheza Barcelona, kuna vitu vichache vyakumjenga ili aweze kuwa bora zaidi
“Umri wake ni mdogo lakini unaona anavyojituma katika klabu hata kikosi cha taifa, anahitaji sapoti ili kufika mbali zaidi na mfano angekuwa katika mataifa ya Ulaya lazima angechezea timu kubwa duniani.


“Hata Mudathir ni mchezaji mzuri kama nilivyotangulia kusema kuna vitu vichache vya kuwajenga, lakini wana uwezo wa kucheza Ulaya,” alisema Amunike.


Alisema Tanzania imebarikiwa wachezaji wazuri ambao wanaweza kuongeza nguvu katika kikosi cha Stars, lakini kitu muhimu wanachohitaji ni maandalizi na mafunzo bora.


Akizungumzia nafasi ya Taifa Stars katika fainali zijazo za mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Misri, alisema mikakati yake ya kuwakabili wapinzani itakuwa wazi baada ya ratiba kupangwa.

“Tunasubiri kwanza makundi yapangwe, baada ya hapo tutajua tunawakabili nani na mikakati ipi itatusaidia kupambana na kufanya vizuri,” alisema Amunike.


Amunike ameiwezesha Taifa Stars kufuzu fainali za Afcon kwa mara ya pili katika historia ya Tanzania, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Uganda na kuvuna pointi nane, katika mchezo wa mwisho uliochezwa wiki moja iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mara ya kwanza, Tanzania ilishiriki fainali hizo mwaka 1980 zilipofanyika nchini Nigeria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles