RAISI Jakaya Kikwete jana aliongoza maelfu ya wananchi katika mazishi wa mwasisi wa chama cha TANU na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM), Peter Kisumo yaliyofanyika katika Kijiji cha Kirongwe wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Ibada ya mazishi ilifanyika katika Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Pare ambako ibada ya mazishi iliongozwa na aliyekuwa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Marth Shao.
Rais Kikwete aliwasili kijijini hapo saa 9:10 kwa kutumia helkopta mbili ambazo zilitua kwa nyakati tofauti katika Uwanja wa Chuo cha Ufundi (UVTC) Mwanga.
Hata hivyo, Rais Kikwete hakuzungumza chochote badala yake Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha Rose Migiro, alizungumza kwa niaba ya CCM na Serikali.
Dk Migiro alisema Kisumo aliishi maisha yaliyotukuka na kwa misingi ya maadili ya utumishi wa umma.
Alisema mzee Kisumo alikuwa mtu wa namna ya pekee ambaye katika ujana wake alifanya kazi katika sekta mbalimbali kwa tija kubwa hivyo kifo chake kimeacha pengo kubwa.
“Mzee Kisumo alikuwa mtumishi mahiri na muadilifu wa serikali na aliteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali za juu serikalini na katika chama cha TANU na baadaye CCM na aliweza kuandika Katiba ya mwaka 1977 pamoja na kujenga kada ya uongozi katika taifa,”alisema Dk. Migiro.