24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mgeja, Guninita waibwaga CCM, wajiunga Chadema

mgeja, guninitaNa Elizabeth Hombo, Dar es Salaam

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja amesema chama hicho kimeacha misingi yake na sasa kimegeuka kuwa kampuni ya familia moja.

Mgeja pia amempiga kijembe mgombea urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli akimfananisha na dereva ambaye hajaweza kuendesha gari vizuri ‘learner’ akimaanisha kuwa hana uwezo wa kukiongoza chama hicho.

Mgeja alitoa kauli hiyo   Dar es Salaam jana alipotangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akifuatana na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita ambaye pia  amejiunga na Chadema.

Mwanasiasa huyo mkongwe aliyepata kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM, alisema ametumika ndani ya chama hicho kwa muda mrefu huku akishiriki kurekebisha kasoro mbalimbali zilizojitokeza lakini sasa imefika mwisho.

“Pamoja na kuzirekebisha kasoro zilizojitokeza mara kadhaa lakini kila jambo lina mwisho wake na kurekebisha mambo hayo nayo inafika mwisho.

“Chama sasa kimekuwa cha BMW, yaani cha baba, mama na watoto, kwa maana hiyo chama kimekuwa cha kampuni au familia ndiyo maana maoni ya wanachama na wananchi yanapuuzwa,”alisema.

Mgeja ambaye   aliongozana na makada wengine wa chama hicho, alisema yeye   na wenyeviti wa mikoa wa CCM takriban 23, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)   na baadhi ya wabunge waliona mabadiliko yanahitajika ndani ya CCM.

“Matatizo ndani ya chama ni makubwa tunastahili tupate dereva fundi kwa sababu sisi tuliokitumikia chama tunakifahamu … hapa tulipofika hivyo kinahitaji ukarabati mkubwa na tulishawishika kuwa Lowassa angeweza kukitoa hapo kilipo.

“Lakini kwa bahati mbaya mawazo ya wanachama na wananchi, mwenyekiti wetu ameyapuuza. Nilikuwa navuta subira angekuwa muungwana angezungumza na kuomba radhi kwa aliyoyafanya kwa sababu  hayavulimiliki, anakuja kwenye vikao vizito akiwa na majina yake mfukoni.

“Tukamwuliza atusomee sifa za hao wagombea watano lakini akafanya ubabe, akatengeneza nguvu kubwa, polisi wakazunguka lile jengo wakiwa na mabomu, farasi, gari ya maji ya washasha na hata ndani ya ukumbi polisi walikuwapo wakiwa na mabomu.

“Nilimwuliza mwenyekiti kwamba leo tuko Burundi? Tunawalalamikia kina Nkurunziza kumbe tunao wengi Tanzania,  tulipekuliwa na vijana wadogo mpaka wakaona na hirizi zetu.

“Taswira ya chama imeondoka, niliona kina Emmanuel Nchimbi walitoka wale hawakuwa wajinga waliona kasoro kubwa imefanyika,”alisema.

Mgeja   alisema chama kimekuwa si kile cha wakati wa Mwalimu Nyerere… kimejaa chuki, rushwa, fitna, kimepoteza mwelekeo na   nguvu zilizotumika wakati wa kumpata mgombea urais ilikuwa hatari sana.

Mwisho

GUNINITA

Naye aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita alisema amezaliwa akiwa CCM na  alikitumikia chama hicho kwa   miaka 35, lakini kutokana na kukiukwa  misingi ameamua kuondoka.

Alisema ni dhahiri   vijana wadogo  wanaowatukana viongozi wenye umri zaidi ya baba zao wametumwa na chama.

“Haiwezekani kijana mdogo anatukana viongozi wakubwa huku chama kikikaa kimya na mwishoni kupata uongozi kwa utaratibu wa uyoga uyoga, sijui laana hii wataipeleka wapi,”alisema Guninita.

Alisema CCM kilipofikia sasa kinakufa kama ilivyokuwa kwa chama cha KANU cha Kenya na UNIP cha Zambia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles