28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Kikwete amlilia Kombani

CelinaNA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

RAIS Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kufuatia kifo cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti na Utumishi wa Umma, Celina Kombani, kilichotokea juzi katika Hospitali ya Apollo nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kugundulika kuwa na saratani.

Rais Kikwete pia amemtumia salamu za pole mume wa marehemu, Swaleh Ahmad Pongolani, watoto, ndugu na jamaa kutokana na msiba huo.

Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilisema marehemu Kombani atakumbukwa kwa kuwa hodari na aliyependa kushirikiana na wenzake na kwamba wamepoteza mama mchapakazi.

“Nimepokea taarifa za kifo cha mama Kombani kwa huzuni kubwa, najua machungu na maumivu mliyonayo kwa kuondokewa na kiungo muhimu katika familia yenu, poleni sana, mama ni nguzo ya familia niko nanyi katika msiba huu mzito kwenu,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alisema pamoja na kwamba kifo hakiepukiki, bado ni kitu ambacho kinashtua, kuhuzunisha na
kuleta unyonge mkubwa kwa wafiwa katika jamii.

“Naungana nanyi katika kipindi hiki kigumu kumuombea Mama Kombani ili Mwenyezi Mungu ampe mapumziko mema ya milele, nawaombea wana familia na ndugu wa marehemu, Mwenyezi Mungu awatie nguvu, uvumilivu na subira katika kipindi hiki, niko nanyi katika kipindi hiki kigumu kwa hali na mali, nawaomba msijisikie wapweke,”
alisema Rais Kikwete.

Mwili wa marehemu Kombani unatarajia kuwasili nchini leo mchana na kuzikwa shambani kwake mkoani Morogoro. Marehemu Kombani alikuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Ulanga Mashariki kwa tiketi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na tayari alikwishalitumikia jimbo hilo kwa kipindi cha miaka 10.

Kombani alizaliwa Juni 19, 1959 na ameacha mume, watoto watano na wajukuu wanne.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles