25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

RAIS KENYATTA AWAOMBA RADHI WAKENYA

NAIROBI, KENYA


RAIS Uhuru Kenyatta wa Kenya alihutubia taifa kupitia kikao cha pamoja cha mabunge yote mawili la taifa na seneta jijini hapa juzi akiomba msamaha kwa Wakenya.

Hotuba ya kiongozi huyo iliyochukua muda wa karibu saa moja, iligusia masuala ya utangamano na umoja wa Taifa huku akiwataka Wakenya wabadilike na kuwa mfano wa kuigwa na mataifa jirani.

Akirejea salamu zake na kinara wa Muungano wa NASA, Raila Odinga Machi 9, 2018, Rais Kenyatta alisema kuna haja ya kila Mkenya katika kila kona ya taifa kuiga mfano wao wa kushikamana na kuhubiri amani.

“Ninaomba msamaha iwapo kwa vyovyote vile nilikosea Taifa katika mazingira ya siasa za uchaguzi wa urais mwaka 2017,” alisema Rais Kenyatta.

Akizungumzia kuhusu mfumo wa uchaguzi wa Kenya, alieleza haja ya wanasiasa kubadili mkondo wao wa namna ya kuziendesha, badala yake wawe wakitumia jukwaa hilo kuhubiri amani na umoja wa taifa.

“Wakati umewadia tubadilishe siasa za chuki na ukabila,” alisisitiza Kenyatta.

Muungano wa upinzani wa Nasa ulioshiriki uchaguzi wa 2017 chini ya kinara wake Raila Odinga ulipinga ushindi wa Rais Kenyatta na Naibu wa Rais, William Ruto.

Kenyatta na Ruto walikuwa wakitetea nyadhifa zao kwa tiketi ya Chama cha Jubilee, ambacho Nasa iliwasilisha malalamiko kupinga ushindi wake wa Agosti 8, 2017 katika Mahakama ya Juu, ambayo iliuharamisha.

Tume Huru ya Uchaguzi na Uratibu wa Mipaka (IEBC) ililazimika kuandaa uchaguzi mpya uliofanyika Oktoba 26, 2017, ambao hata hivyo NASA iliususia.

Rais Kenyatta kwenye hotuba yake kwa Taifa pia alisema viongozi na wanasiasa wakiiga siasa za amani, mataifa jirani yataiga mkondo wa Kenya.

Baada ya kula kiapo Novemba 28, 2017, Kenyatta aliweka wazi kuwa awamu yake ya pili na ya mwisho itazingatia ajenda kuu nne.

Ajenda hizo ni kuangazia usalama wa chakula, makazi bora na nafuu, ujenzi wa viwanda ili kukabiliana na ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, na matibabu bora.

Aidha, Kenyatta alieleza azma yake katika kuafikia ajenda hizo na kuwaomba magavana kumsaidia kuzifikia.

Alisema msimu wa siasa umeisha na huu ni wakati wa viongozi waliochaguliwa Agosti 8 kutekeleza miradi ya maendeleo waliyoahidi Wakenya.

Rais pia alisisitiza kuwa maendeleo hayo hayatajiri iwapo viongozi hai hawatapigana na donda ndugu la ufisadi.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Rais, maspika wa mabunge yote mawili, mawaziri, makatibu, baadhi ya magavana na maseneta, wabunge, mabalozi kadhaa wa nchi za kigeni, wanadiplomasia waalikwa kutoka nchi za nje, na viongozi wengine mashuhuri serikalini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles