NAIROBI, Kenya
RAIS Uhuru Kenyatta wa Kenya, amesema Serikali yake itatoa msaada wa mabati, mablanketi na magodoro kwa waathirika wote wa tukio la tetemeko la ardhi lililotokea Jumamosi iliyopita mkoani Kagera.
Taarifa iliyochapishwa na gazeti la Daily Nation la Kenya jana jioni, ilisema msaada huo unatarajia kusafirishwa leo kwenda kwa waathirika wa tetemeko hilo kwa ndege ya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF).
Taarifa hiyo ilisema jana hiyo hiyo, Rais Kenyatta alimpigia simu Rais Dk. John Magufuli kumpa pole na kuonyesha mshikamano na Serikali ya Tanzania na raia wake kutokana na upotevu wa maisha, majeruhi na uharibifu wa mali uliosababishwa na tetemeko hilo.
“Nimesikia kwa masikitiko makubwa upotevu wa maisha ya watu 16, majeruhi ya mamia ya watu kwa kaka na dada zetu wa Tanzania pamoja na uharibifu mkubwa wa mali na ustawi wa jamii kutokana na tetemeko baya la ardhi lililotokea wilayani Bukoba, kaskazini magharibi mwa Tanzania.
“Kwa niaba yangu binafsi, Serikali na watu wa Kenya, natuma salamu zangu za dhati za rambirambi kwako, Serikali na watu wa Tanzania na hasa familia za waathirika,”alisema.
Rais Kenyatta aliwaombea majeruhi wapone haraka pamoja na kuzitakia faraja familia zilizopoteza wapendwa wao kuwa na subira
MBOWE
Katika hatua nyingine, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jana kimetoa mkono wa pole kwa waathirika wa tetememo hilo.
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe akiwa na Mbunge wa Bukoba Mjini, Willfredy Rwakatale na Mbunge wa Viti Maalumu wa CUF, Saverina Mwijage walitoa mkono wa mkoano wa pole wa Sh milioni 2.1.
Mbowe alisema msaada huo, utagawiwa kwa kaya 16 ambazo zimepoteza ndugu, huku kila kaya ikipewa kilo 50 za mchele na sukari kilo 25u.
Pia Mbowe alitoa simenti mifuko 150 katika kata ya Kahororo kwa familia 15 ambazo zimepoteza makazi, ambapo kila yaka itapewa mifuko 10.
“Ndugu zangu tukio hili sio la Serikali au la chama chochote, ni jambo la kitaifa,Serikali inapaswa kutenga fungu kubwa kwa ajili ya kuisaidia jamii,”alisema.
Pia alitemberea Shule ya Sekondari Ihungo na kuwapo pole wanafunzi ambao hivi sasa wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na kukosa madarasa.
Alisema kutokana na hali inavyoonekana katika shule hiyo, si la kufumbia macho kwani litakapoachwa tu na wanafunzi wakaendelea kusomea katika madarasa hayo yawezekana kutokea maafa makubwa zaidi.
“Jamani katika hili hakuna anae takiwa kumtupia mtu yeyote lawama katika hili, hakuna habari za chama chochote cha kisiasa au kumtupiana mpira, hii ni mitihani ya Mungu tushirikiane kwa pamoja”alisema Mbowe.
Baada ya kuonekana ameguzwa na tukio hilo, Mbowe alitoa ng’ombe mmoja kwa ajiri ya kitoweo kwa wanafunzi hao.
Naye Saverina Mwijage, alisema tukio linapaswa kuwaunganisha watu wote bila kujali itikadi za kisiasa.
“Hili ni jambo la kitaifa,watoto na akina mama wanalala nje, tuache mambo yote tuwasaidie ili kuwajengea mahema kwa ajiri ya kulala tuache kupiga kelele zisizo na manufaa kwa wananchi,”alisema Mwijage