NAIROBI, KENYA
RAIS Uhuru Kenyatta wa Kenya, amepiga marufuku matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kutoa amri ya kuzuia miradi yote mipya ya maendeleo nchini humo.
Akizungumza juzi katika ukumbi wa Kenyatta International Convention Centre na makatibu wakuu, wakurugenzi, makamu wakuu wa vyuo vya umma na wenyeviti wa mashirika ya umma, Rais Kenyatta ametoa amri hiyo kwa taasisi zote za umma kutoanzisha miradi mipya ya maendeleo hadi ile iliyopo itakapokamilika.
Ameongeza kuwa miradi yote mipya ya maendeleo ikifanyika tangu kutolewa amri hiyo na bila idhini ya Hazina ni kosa ambalo adhabu yake ni kufukuzwa kazi kwa ofisa yeyote.
“Hakutaanzishwa mradi mpya sasa hadi mtakapokamilisha le iliyopo. Kama hamtamaliza kwa wakati hiyo ni juu yenu, lakini lazima mmalize kwanza ndipo mtaruhusiwa kuanzisha mipya. Miradi itakayoruhusiwa ni ile iliyopo kwenye ajenda nne za maendeleo, lakini hata hiyo nayo inatakiwa kuidhinishwa na makatibu wakuu au wakurugenzi wa Hazina,” alisema Kenyatta.
Rais huyo aliwaonya maofisa wa Serikali wote watakaojichukulia amri mkononi kuanzisha na kuendelea na miradi mipya kabla ya kumaliza ile iliyopo kwa wakati huu na bila kibali cha mamlaka ambako hatua zote muhimu ikiwemo mamlaka ya ununuzi itahusika kupitisha.