23.9 C
Dar es Salaam
Sunday, April 21, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Kagame anguruma

Paul Kagame
Rais wa Rwanda, Paul Kagame

Na Mwandishi Wetu, Kigali

RAIS wa Rwanda, Paul Kagame, amenguruma tena na kusema atakuwa karibu na nchi yenye masilahi kwa nchi yake.

Amesema suala la uhusiano wa nchi nyingine linategemea ukaribu kwani kila Taifa linahitajiana na mwenzake.

Kwa mujibu wa mtandao wa Chimpreports, kauli hiyo aliitoa juzi katika Mdahalo na Vijana wa Afrika ulioandaliwa na Taasisi ya Mafunzo ya Maendeleo ya Mandela mjini Kigali, Rwanda ambapo aliweka wazi mikakati ya Serikali yake na nchi jirani pamoja na fursa za vijana katika kupata keki ya Taifa.

“Kwa kadiri ya unavyokuwa na mwenzako wa karibu ndivyo mnavyozidi kuhitajiana. Kama majirani, kila mtu anamhitaji mwenzake,” alisema Rais Kagame.

Pamoja na hatua hiyo aliwataka vijana kujiamini katika kudai mgao wao katika kuifaidi keki ya taifa na kupinga uongozi mbaya.

Alisema rushwa inabakia kuwa moja ya sababu ya bara la Afrika kubakia nyuma kimaendeleo na kitendo na hatua hiyo inapaswa kupingwa kwa nguvu zote.

“Kwanini rasilimali ziwe laana? Ukosefu wa rasilimali ndio unaopaswa kuwa laana.

“Vijana wanapaswa kupambana na rushwa kwa kutokuwa tayari kujihusisha nayo. Wekeni mbele tamaa ya mafanikio kwa kufanya mambo yenye heshima,” alisema Rais Kagame.

Rais Kagame alisema vijana wanapaswa wasiridhishwe na kasi ya maendeleo ya Afrika.

“Swali ni nini tunafanya ili kusonga mbele? Tumekubaliana na utamaduni wa kuwaangalia wengine na si kujiangalia wenyewe kwa ajili ya utafutaji suluhu … Mnahitaji kuwa wabishi. Wakati viongozi wanaendelea na mwenendo wenye kuwasababishia matatizo, ninyi mnatakiwa kuwa katika hali inayosukuma mambo ili kieleweke,” alisema Kagame.

Kuhusu namna vijana wanavyoweza kutumia uwezo na vipaji vyao, Kagame alisema: “Tunatumiaje vipaji tulivyo navyo katika chumba hiki? Inaanzia kwa kutaka kuwa na msaada na manufaa kwa jamii.”

Aliongeza: “Msiba ulioipata Rwanda unapaswa kuwa somo kwetu. Hatuwezi kutafuta suluhu kwingine. Kwanini tujiruhusu kuwa waathirika walionaswa katika vita baina ya Mashariki na Magharibi kwa ajili ya rasilimali zetu,” alisema na kuhoji.

Rais Kagame pia aligusia kwamba, kuwa na ujuzi hakutoshi kwa kuwaeleza kuwa kujua si mwisho wa matatizo ila lengo la ujuzi ni namna wa kuutumia ili ulete mafanikio yanayokusudiwa.

Kauli hiyo ya Kagame ambayo ilionekana kusisimua na kuwahamasisha vijana kuwataka viongozi wao watoe huduma bora kwa umma na kusema Afrika inapaswa kuacha kutegemea magharibi kwa maendeleo yake.

“Tunaweza kusubiri kwa miaka mingine 100 iwapo tutaendelea kufikiria kwamba walipa kodi wa Magharibi wanahusika na maendeleo yetu,” alisema Kagame.

Mdahalo wa Vijana wa Afrika unaofanyika kila mwaka unazungumzia chaguzi na uongozi unakusudia kuongeza idadi ya vijana wanaoshiriki kikamilifu katika chaguzi za Afrika na michakato ya uongozi kwa amani.

Kutokana na hali hiyo, huchukuliwa kama jukwaa muhimu ambalo vijana wa Afrika ambao hupata fursa ya kuchangamana wakati wakihoji na kuongeza uelewa wa masuala ya masilahi ya pande zote yahusuyo maendeleo na mabadiliko yanayostawisha bara la Afrika.

Washiriki walitoka kanda zote za Afrika, Kaskazini, Magharibi, Kati, Mashariki na Kusini mwa Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles