Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha mwandishi wa habari mkongwe na mhadhiri mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Nkwabi Ng’wanakilala.
Katika salamu ambazo amemtumia Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema kifo hicho kimelinyang’anya taifa mmoja wa wanataaluma wa habari mahiri na mtumishi hodari wa umma ambaye alithibitisha sifa hizo katika nafasi zote alizozishikilia.
“Alithibitisha sifa hizo kwenye nafasi ya Ukurugenzi wa Idara ya Habari, kwenye Ukurugenzi wa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na kwenye Ukurugenzi wa Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA). Tasnia ya habari imepoteza kiongozi hodari,” alisema Rais Kikwete.
Ng’wanakilala alifariki dunia mwishoni mwa wiki kwenye Hospitali ya Rufani ya Bugando mjini Mwanza kwa matatizo ya figo na tumbo na alizikwa juzi nyumbani kwake Kibamba, Dar es Salaam.