WASHINGTON DC, Marekani
RAIS zamani wa nchi hii, George HW Bush anatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwake Jimboni Texas katika eneo ambalo alizikwa mkewe,Barbra.
Kabla ya mazishi hayo ya leo jana viongozi kutoka mataifa mbalimbali walihudhuria ibada maalum ya kuuombea mwili wa kiongozi huyo iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Washington ambako ulipelekwa baada ya kuondolewa katika Jengo la Bunge la nchi hii.
Habari zilizopatikana mjini hapa zinaeleza kwamba miongoni mwa viongozi waliohudhuria ibada hiyo ni pamoja na Rais Donald Trump na watangulizi wake, Barack Obama, Bill Clinton na Jimmy Carter.
Mbali na viongozi hao, taarifa hizo ziliwataja wengine kuwa ni Prince wa Wales, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel Mfalme na Jordan, Abdullah II na Waziri Mkuu wa zamani John Major.
Kiongozi huyo ambaye aliitumikia nchini kama rais wa 41 kati ya mwaka 1989 na 1993, alifariki Ijumaa wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 94.
Tangu alipofariki kumekwapo na shughuli mbalimbali za kuuaga mwili huo ambazo zilianza Jumatatu wiki hii kwa kuhamisha mwili huo kutoka Jimboni Texas hadi hapa kwa ajili ya kuwapa fursa viongozi na raia kuweza kutoka heshima hizo.
Jana pia ilikuwa ni siku ya maombolezo kitaifa ambapo ofisi nyingi za serikali zilifungwa likiwamo pia soko la hisa.