ASUNCION, PARAQUAY
RAIS wa Paraguay, Horacio Cartes, amemfukuza kazi Waziri wa Mambo ya Ndani, Miguel Tadeo Rojas na Mkuu wa Polisi, Crispulo Sotelo kufuatia maandamano yaliyoambatana na vurugu kusababisha kifo cha mwanaharakati Rodrigo Quintana.
Quintana (25), ambaye ni kiongozi wa tawi la vijana la chama cha upinzani cha Kiliberali alipigwa risasi na polisi juzi asubuhi wakati walipofanya msako katika ofisi za chama hicho wakiwatafuta waandamanaji.
Kiasi ya watu 30 walijeruhiwa wakiwemo wabunge watatu.
Polisi ilisema watu 211 walikamatwa miongoni mwao wakiwa watoto.
Waandamanaji walivamia majengo ya bunge na kuliwasha moto siku ya Ijumaa wakipinga hatua ya Bunge la Seneti kukutana kwa faragha na kupitisha muswada wa kufanyia marekebisho kipengele cha Katiba kumruhusu Rais Cartes kuwania muhula wa pili madarakani.
Paraguay ilipiga marufuku marais kugombea muhula mwingine tangu mwaka 1992 kuepusha kurejea kwa tawala za kidikteta kama wa Jenerali Alfredo Stroessner aliyeitawala nchi hiyo kuanzia mwaka 1954 hadi 1989.