KITALE, KENYA
RAIS Uhuru Kenyatta akiwa katika kampeni zake mjini Kitale akiwaomba wenyeji kumpigia kura aingie Ikulu kwa muhula wa pili na wa mwisho amelitaka Gereza la Kitale litoe ekari 1,000 za ardhi kwa wenyeji ili wapanue mji wao.
“Hatua hii inatokana na mapenzi yangu kwa wenyeji wa Mji wa Kitale na ambao ningetaka kuona wakifikia malengo yao ya uwekezaji ndani ya mji mkubwa,” alisema Rais Kenyatta akihutubia juzi.
Amesema kuanzia wiki ijayo, kabla ya uchaguzi mkuu Agosti 8, 2017, ekari hizo zitakuwa tayari kukabidhiwa kwa wenyeji.
Hata hivyo haijulikana namna vipande hivyo vya ardhi vitakavyogawanywa.
Rais Kenyatta pia alimpigia debe mgombea ugavana kwa tiketi ya Chama cha Jubilee, Maurice Kakai, akisema, “Huyu ndiye atakayepewa jukumu la kupanga mji mpya wa Kitale na ulio na nafasi pana ya kuandaa nafasi za ajira kwa wenyeji.”