NAIROBI, KENYA
KIONGOZI wa Muungano wa Upinzani wa National Super Alliance (NASA), Raila Odinga, amepuuza onyo la Serikali kuwa anaweza kuhukumiwa kunyongwa kwa uhaini, akiapishwa kuwa ‘Rais wa Wananchi.’
Akihutubia katika Kijiji cha Kyondoni, Kitui Magharibi juzi wakati wa mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa eneo hilo, Francis Nyenze, Raila alisema mbele ya kupigania haki haogopi kifo.
“Tulisema tulishinda uchaguzi ule na hivyo tutaapishwa. Tumeambiwa ati ooh uhaini, uhaini, ati hicho ni kifo. Mimi nataka kumjibu Githu Muigai (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) hapa na bosi wake (Rais Uhuru Kenyatta). Ikiwa ni lazima kifo kitokee ili kuzuia wizi wa kura huko mbele, tutaapishwa ili tufe,” alisema Raila.
Kauli yake inakuja baada ya Mwanasheria Mkuu, Profesa Githu Muigai kumuonya dhidi ya kuapishwa akisema kuwa anajitafutia kifo na kumshauri asipotoshwe na baadhi ya mawakili na wanasiasa wanaomzunguka katika NASA.
Kinara mwingine wa NASA, ambaye ni kiongozi wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, hakudhuhuria mazishi hayo, washirika wake wakisema kuwa ndege aliyopanga kusafiria ilichelewa.
Juzi Jumanne, Raila na vinara wenza wa NASA, Moses Wetangula na Musalia Mudavadi, walisisitiza kuwa walipokonywa ushindi kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 8.
“Wakenya wanataka haki itendeke katika uchaguzi, mageuzi katika kikosi cha polisi na mahakama huru ambayo haitaweza kutishwa na walio mamlakani,” alisema Raila.
Alisema kama NASA haingekuwa imeshinda uchaguzi wa Agosti 8, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ingefungua data zake kama ilivyoagizwa na Mahakama ya Juu.
“Mahakama ya Juu ilibatilisha matokeo ya kura ya urais na ikaagiza IEBC kufungua data zake tukague, lakini ilikaidi agizo hilo,” alisema Raila.
Awali akizungumza mjini Kilifi mwishoni mwa wiki kwenye kikao cha kwanza cha Bunge la Wananchi eneo la Pwani, Raila alisema yuko tayari kuapishwa.
“Niko tayari kuinua Biblia. Nitainua Biblia, ni heri kuamini jambo na kulisimamia kuliko kushindwa kulifanya,” alisema Raila akiwaambia viongozi wa NASA eneo la Pwani.
Akihutubia wakati wa mazishi hayo, Mudavadi aliilaumu Serikali ya Jubilee kwa kutokubali kukosolewa.
Alishangaa jinsi Rais Uhuru anavyoweza kumshauri Jaji Mkuu David Maraga kukubali kukosolewa ilhali anakataa kukubali polisi wanaua Wakenya wasio na hatia.
Kiongozi wa Wachache Bungeni, John Mbadi, alikosoa wanaopinga Raila kuapishwa, akisema hawajui uchungu wa kunyang’anywa ushindi.
“Tunajua mlimpigia kura, tutamwapisha hata kama tunatishwa, hatuogopi kitu ili mradi haki inapatikana,” alisema Mbadi.