27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

RAILA: HATUKO TAYARI KUGAWANA MADARAKA NA WEZI

NAIROBI, KENYA

KIONGOZI wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, amesema muungano wake wa NASA hautagawana madaraka na aliowaita wezi, siku mbili baada ya Mahakama ya Juu kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais wa mwezi uliopita.

Uchaguzi mpya utaitishwa ndani ya siku 60 tangu kutolewa kwa uamuzi huo wa mahakama.

Raila alikuwa akipuuza madai yaliyotolewa na Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, William Ruto kuwa amelenga kushinikiza kuundwa kwa Serikali ya ushirika.

“Tunataka Serikali nzima, tutashinda uchaguzi wa rais na tutashinda mapema. Hatuwezi kugawana madaraka na wezi. Kenyatta, achana na Wakenya,” alisema katika mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Masinde Muliro huko Mathare jana.

Katika mkutano huo, Raila alisindikizwa na mgombea wake mwenza, Kalonzo Musyoka, Kiongozi wa Chama cha ANC, Musalia Mudavadi na Seneta wa Bungoma, Moses Wetangula.

Raila, ambaye pia aliwania urais mwaka 1997, 2007 na 2013 bila mafanikio, alirudia kauli yake kuwa baada ya uamuzi wa mahakama, hawatashiriki uchaguzi wa marudio bila makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Ijumaa alitoa wito kwa makamishna wa IEBC kujiuzulu na kushtakiwa mahakamani kwa uhalifu na kusababisha hasara kwa taifa.

Hata hivyo, Kenyatta kwa upande wake amesisitiza uchaguzi ufanyike chini ya tume ile ile vinginevyo Mahakama ya Juu nayo ivunjwe kwa kile alichodai kuwa ya kihalifu.

Ijapokuwa Kenyatta aliahidi kuheshimu uamuzi wa mahakama licha ya kutokubaliana nao, amekuwa akiishambulia huku akiwaita majaji kuwa ni wakora.

Aidha wakati akihutubia mkutano katika Kaunti ya Nakuru juzi, alisema Raila anafahamu atashindwa vibaya, hivyo anachotafuta sasa ni kuingia madarakani kwa mlango wa nyuma.

Kabla ya kusafiri kwenda Nakuru, awali Kenyatta alihutubia mkutano wa magavana, maseneta, wawakilishi wanawake na madiwani waliochaguliwa kwa tiketi ya chama chake cha Jubilee Ikulu mjini hapa.

Katika mkutano huo, alisisitiza kutokubaliana na hukumu hiyo, akitolea mfano kuwa wingi wa viongozi hao wa kuchaguliwa kupitia chama chake ni ushahidi tosha kuwa alishinda uchaguzi wa Agosti 8.

“Hii mahakama imekula njama na watu hawa, ambao hawana nia na uchaguzi. Wanachotaka si kingine zaidi ‘nusu mkate’,” alisema akimaanisha Serikali ya ushirika.

Aidha alitangaza kuwa timu yake haina muda wa kupoteza bali kuendelea na kampeni nchi nzima.

Uamuzi wa Mahakama ya Juu wa Ijumaa iliyopita kwamba IEBC ilifanya madudu, ulibatilisha ushindi wa Rais Kenyatta, ambao ulihusisha pengo la kura milioni 1.4 dhidi ya Raila.

Hukumu hiyo inaanzisha mchuano mpya baina ya Kenyatta (55) na mwanasiasa mkongwe Raila (72) na shinikizo baina ya pande mbili limeshaanza kupanda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles