29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Raila apokewa vibaya katika ngome yake

KISUMU, KENYA

WAKAZI wa Muhoroni katika Kaunti ya Kisumu, juzi Jumatatu walimpokea kwa mabango ya kumpinga kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga alipoenda kuzindua mradi wa viwanda eneo hilo.


Wakibeba mabango na kuandamana, wakazi hao walilalamika Serikali inataka kutwaa ardhi yao kwa nguvu ili kujenga mradi huo, wakisisitiza hawauungi mkono na kwamba hawakushauriwa kabla ya uamuzi huo kufikiwa.


Hatua hiyo ya mapokezi mabaya kwa Odinga ilikuwa ya kushangaza katika ngome yake kisiasa, ambako amekuwa akiheshimika kwa miaka mingi na maamuzi yake kupokewa bila maswali.


Vioja vilianza wakati Odinga aliposema ujenzi wa mradi huo wa kiuchumi una umuhimu kuliko kuacha ardhi hiyo kuendelea kutumiwa kwa kilimo.
Mara baada ya kutamka hayo, wakazi walimkemea na kupiga kelele, wakisema wanataka kuachiwa ardhi yao badala ya ujenzi wa mradi huo.
“Kwanini mnaniaibisha? Ninaleta maendeleo ilhali hamuoni miradi ambayo itawafaidisha,” Odinga alisema akishangaa.


Hata hivyo, vijana hao walivurumishiwa viboko na watu wanaounga mkono ujenzi wa mradi huo na mabango yao yakaharibiwa, huku Odinga akijaribu kutuliza hali na kuwasihi wakazi hao kuukubali mradi huo.


Odinga alisema mradi huo utajengwa katika ardhi ya ekari 500 na ujenzi utaanza mara tu Sh milioni 500 za Kenya zitakapotolewa na Serikali baadaye mwaka huu, huku Sh bilioni 2.5 zikitarajiwa kutolewa mwaka ujao.


“Rais Uhuru Kenyatta, Rais wa Uganda Yoweri Museveni na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Felix Tshisekedi wanatarajiwa kuzindua rasmi ujenzi wa mradi huo Agosti mwaka huu,” alisema Odinga.


Alikuwa ameandamana na mawaziri Peter Munya wa Biashara na Viwanda, James Macharia wa Uchukuzi na John Munyes wa Madini.
Hata hivyo, hilo limekuja siku chache tu baada ya yeye na Rais Uhuru Kenyatta kurejea mikono mitupu kutoka China ambako walienda kutafuta mkopo wa kuendeleza ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) hadi Kisumu, badala yake kuahidiwa ujenzi huo.


“Reli mpya ya SGR itajengwa kutoka Naivasha, Narok, Bomet, Sondu hadi Kisumu,” Odinga aliwaeleza wakazi wa Sondu kabla ya kuandamana na Rais Kenyatta nchini China kuomba mkopo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles