NAIROBI, KENYA
KIONGOZI wa Muungano wa Upinzani nchini Kenya, NASA, Raila Odinga, amepinga marudio ya uchaguzi katika majimbo manne ya ukanda wa Nyanza ambayo hayakushiriki zoezi hilo kutokana na vurugu zilizozuka miongoni mwa wananchi, huku idadi kubwa ikisusa kupiga kura. Mwenyekiti wa Tume IEBC, Wafula Chebukati, alitaja Kaunti ambazo zimeathirika ni Siaya, Migori, Kisumu na Homa Bay kuwa yatafanya uchaguzi wake leo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na kituo cha runinga cha Citizen, Odinga amesema kuwa uamuzi uliofanywa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC kuahirisha uchaguzi katika ukanda wa Nyanza hadi Oktoba 28(leo), haukubaliki hivyo ameamua kuwahamasisha wafuasi wake badala ya kupiga kura wataandamana.
“Kufanya marudio ya uchaguzi katika Kaunti 4 ya Luo Nyanza ni unyanyapaa wa kikabila. Hakukuwa na uchaguzi katika kaunti nyingi za humu nchini, toshekeni na kura sufuri,” alisema Raila.
Amesisitiza kuwa uchaguzi wa marudio ya urais haujahusisha wananchi wote wa Kenya na kuwaomba wafuasi wake kulinda amani katika kipindi hiki anachotafuta suluhisho la kudumu.
Odinga amesema kuwa atakabiliana na matatizo yote yanayotokea sasa ndani ya upinzani pamoja na nchi kwa ujumla.
Katika mazungumzo hayo na Citizen, Odinga aliituhumu kampuni moja ambayo hakuitaja jina kwa madai ya kushirikiana na Chama cha Jubilee kuvuruga taratibu za uchaguzi, ikiwamo wizi wa kura, jambo ambalo ametishia kuwa anaweza kuitisha maandamano dhidi ya bidhaa zao.
Kinara huyo wa upinzani amesisitiza kuwa muungano wao hautambui uchaguzi wa marudio uliofanyika Oktoba 26 na kusababisha vurugu kwenye baadhi ya maeneo nchini humo.
Amesema sababu nyingine ya kutoutambua uchaguzi wa Oktoba 26 zinatokana na sheria ya uchaguzi ambayo inaagiza ufanyike ndani ya siku 90 mara baada ya Mahakama ya Juu kufuta matokeo ya uchaguzi wa Agosti 8, mwaka huu uliompa ushindi mgombea wa Jubilee, Uhuru Kenyatta.
Kwa upande wake kiongozi mwingine wa NASA, Musalia Mudavadi, amesema haikubaliki kurudia uchaguzi katika maeneo ya Kisumu, Migori, Homa Bay na Siaya kwa sababu utavuruga waumini wanaoabudu siku hiyo.
Mudavadi ameomba IEBC kusitisha zoezi la uchaguzi lililopangwa kufanyika leo katika maeneo hayo na kuituhumu Serikali kupanga njama na mikakati mibaya dhidi ya maeneo hayo, ambayo yameonyesha msimamo thabiti kusimama na mgombea wao, Raila Odinga.
KANISA LAMSHUKIA CHEBUKATI
Hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya IEBC, Wafula Chebukati kuratibu upya zoezi la kura ya marudio katika Kaunti za Nyanza ili kufanyika leo, imewakasirisha waumuni wa Kanisa la Seventh Day Adventist (SDA).
Kanisa hilo limemwandikia barua Chebukati likimtaka kuratibu upya tarehe hiyo ili kuwaruhusu waumini kushiriki ibada. Kanisa la SDA Kenya, lina wafuasi zaidi ya milioni tatu.
“Tunataka kukufahamisha kuwa, tarehe hii ni Jumamosi, ambayo ni siku ya maombi kwa waumini wetu zaidi ya milioni tatu Kenya. Hii itawanyima haki yao ya kupiga kura,” ilisema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na kiongozi wa SDA, Samuel Makori.
Tume ya IEBC ililazimika kuahirisha zoezi hilo baada ya wakazi kuzuia shughuli za upigaji kura kuendelea katika kaunti hizo.
WAFUASI WA NASA LONDON WAANDAMANA
Karibia wafuasi 70 wa Upinzani walilazimisha Ubalozi wa Kenya nchini Uingereza, kufunga milango yake mapema Oktoba 26, baada ya wafuasi hao kufika kulalamikia zoezi waliloliita uchaguzi usioaminiwa Kenya.
Kwa mujibu wa gazeti la The Standard toleo la jana, lilisema wafuasi wa NASA walibeba mabango na ujumbe uliomtaka Rais Uhuru Kenyatta kuondoka ofisini, kabla ya bendera ndani ya ubalozi huo kuteremshwa na ofisi kufungwa.
Maandamanao mengine yaliyoshuhudiwa Marekani na Uingereza ya wafuasi wa Jubilee na NASA wakitoa hisia zao.
“Tuliona tu bendera ya taifa ikiteremshwa na mlango wa kuingia kufungwa tulipoanza kujikusanya nje,” alisema Geroge Osore aliyeyaongoza maandamano hayo akiliambia gazeti la Standard.
Osore amesema hawaungi mkono mauaji ya Wakenya wanaoandamana yanayotekelezwa na polisi na kulitaka jeshi hilo kuacha mara moja kutumia risasi dhidi ya waandamanaji.
Ameongeza kwa kusema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilikuwa imeendesha zoezi lisilokuwa na uaminifu. Walitaka Uingereza kuingilia kati hali ya kisiasa ya sasa nchini.
UCHAGUZI WAPINGWA MAHAKAMANI
Katika hatua nyingine, kesi ya kupinga uchaguzi wa marudio imefunguliwa katika Mahakama ya Juu zaidi na Mwanaharakati Okiya Omtata. Katika kesi hiyo, Omtata ameshtaki IEBC na kuomba uchaguzi uliofanyika Oktoba 26, ufutwe kwa mujibu wa Ibara za 138(8) (b) na 138(9) ya Katiba.
Kwa mujibu wa Omtata, uchaguzi wa marudio uliofanyika Oktoba 26 si halali kwakuwa unakiuka kanuni na sheria, hivyo unazo sifa zote za kutoitwa uchaguzi na ufutwe kwa sababu umechangia mgombea wa NASA kujitoa kwenye kinyang’anyiro.
“Viongozi wa Tume ndiyo waliosimamia uchaguzi wa Agosti 8 ambao haukuwa huru na haki pamoja na ukiukwaji wa sheria, ni wale wale wamesimamia uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26 mwaka huu, hivyo unasababisha matokeo ya uchaguzi yanapotangazwa kutoaminika na kutokuwa na maana. Uchaguzi wa Oktoba 26 umeliachia doa taifa letu ambalo limegawanyika katikati, huku ukiukwaji wa Katiba ya mwaka 2010 ukifanyika wazi wazi,” ilisema sehemu ya pingamizi la mwanaharakati huyo.
Katika kesi hiyo amewashtaki Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Wafula Chebukati na wagombea nane walioshiriki uchaguzi wa marudio Oktoba 26.