25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

RAILA AKERA WAFUASI WAKE KWA KUFUTA TUKIO LA KUMWAPISHA

NAIROBI, KENYA


BAADHI ya wafuasi wa upinzani wa National Super Alliance (Nasa), wameeleza hasira zao baada ya kiongozi wa muungano huo, Raila Odinga kufuta mpango wake wa kumwapisha kama ‘Rais wa Watu.’

Odinga na mgombea wake mwenza katika uchaguzi wa Agosti 8,  Kalonzo Musyoka walikuwa waapishwe kuwa rais na naibu rais leo.

Viapo hivyo vilikuwa viende sambamba na maadhimisho ya Siku ya Jamhuri, ambayo yanakumbushia wakati Kenya ilipotangazwa kuwa jamhuri mwaka 1964.

Pamoja na kwamba Odinga na maofisa wengine wa Nasa walidai kuahirisha shughuli hiyo hakumaanishi kuachana na harakati zao za kudai haki katika mfumo wa uchaguzi, baadhi ya wafuasi wa Nasa hawakufurahishwa.

“Nilikuwa nikisubiri tukio hili kwa hamu kubwa. Nilitaka baba akiapishwa kwa sababu naamini ni rais wangu. Hapa ameniangusha kwa uamuzi wake,” alisema mkazi wa Migori, Victor Omondi.

Dishon Hamisi, ambaye ni mfanyabiashara katika mji huo, alisema Nasa imemnyima sababu ya kufurahia Siku ya Jamhuri.

“Niliisubiri kwa hamu kubwa Siku ya Jamhuri kwa sababu nilitaka kusherehekea rais wangu. Sasa hilo halitatokea tena. Sina furaha na sina muda tena na matukio ya Nasa.”

Migori ilikuwa moja ya kaunti nne za Nyanza, ambako wafuasi wa Nasa waliendesha maandamano kupinga marudio ya uchaguzi wa Oktoba 26, wakiishinikiza Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iufute.

Magenge ya vijana yaliweka vizuizi barabarani kuzuia maofisa wa IEBC wasiwasilishe vifaa vya uchaguzi, hali iliyosababisha usifanyike.

Aidha wengine wengi walienda mitandao ya jamii kueleza kuchukizwa kwa uamuzi huo, baadhi wakiituhumu Nasa kwa woga.

Moses Murimi Masiaga, ambaye aliwania Ubunge wa Kuria West kwa tiketi ya Nasa ametangaza kujitoa kutoka muungano huo mara baada ya kinara mwingine wa upinzani. Musalia Mudavadi kusoma tangazo la kuahirisha shughuli ya kuapishwa juzi jioni.

 

“Nimejitoa kuiunga mkono Nasa. Bora niangalie kwingine. Afadhari niwe mgombea huru kuliko kuunga mkono ushirika ambao daima unaniangusha,” Masiaga aliandika katika ukurasa wake wa Facebook.

Mudavadi alisema hatua hiyo imetokana na mashauriano katika muungano huo baada ya kuzungumza na jamii ya kimataifa na wadau wengine hapa nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles