25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

MKUU WA MAJESHI AELEZEA HALI ZA MAJERUHI DRC

AGATHA CHARLES na TUNU NASSOR


MKUU wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo, amesema hali ya askari waliojeruhiwa wakiwa kwenye kikosi cha kulinda amani   Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inaendelea vizuri.

Pia amesema askari mmoja kati ya wawili waliokuwa hawajulikani walipo kutokana na shambulio hilo, amepatikana.

Jenerali Mabeyo aliyasema hayo  Dar es Salaam jana, wakati wa kupokea miili ya wanajeshi 14 waliouawa mwishoni mwa wiki iliyopita wakiwa kwenye kikosi cha kulinda amani   DRC.

“Hali za majeruhi ni nzuri, wanaendelea na matibabu huko, wapo walioumia zaidi wanaotibiwa Kinshasa na wenye hali mbaya zaidi walipelekwa Uganda. Wale wawili waliokuwa wamepotea, mmoja amepatikana,” alisema Jenerali Mabeyo.

Akizungumzia kama tukio hilo litawarudisha nyuma katika kupeleka majeshi ya Tanzania kulinda amani katika nchi mbalimbal duniani, alisema tukio hilo haliwakatishi tamaa kwa kuwa ni moja ya kazi zao.

“Hatujakata tama kwa sababu matukio kama haya ni moja ya kazi zetu. Sisi ni wanachama wa Umoja wa Mataifa na ni jukumu letu kulinda usalama,” alisema Jenerali Mabeyo.

Akizungumzia uimara wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jenerali Mabeyo alisema liko imara ila kikundi cha waasi wa Allied Democratic Forces  (ADF) kilichosababisha vifo hivyo, siyo kikubwa bali kiliwashambulia askari hao kwa kuwa kiko hapo kwa mashambulio.

“Si kikundi kikubwa sana, wao wapo kwa ajili ya kupigana, sisi tupo kwa ajili ya kulinda amani. Hakuna hofu, unaposhambuliwa unajitathimini kwa kilichotokea na kusonga mbele,” alisema Jenerali Mabeyo.

Kwa mujibu wa Jenerali Mabeyo, tukio hilo ni kubwa kutokea ndani ya miaka mitano tangu JWTZ ilipoanza kulinda amani  DRC.

Naye Waziri wa Ulinzi, Dk. Hussein Mwinyi, ambaye alikuwa uwanjani hapo kuongoza mapokezi ya miili hiyo, alisema tukio hilo lilikuwa la kushtukiza, lakini haliondoi nia ya nchi kulinda amani.

“Hili ni tukio la kushtukiza, tunaendelea kulinda amani kwa sababu haya ni matukio yanayotokea mara moja moja. Uimara wa jeshi upo kwa sababu  linafanya kazi kwa weledi.

“Kila juhudi zitachukuliwa   tukio kama hilo lisitokee tena, tuko kule kulinda na tutaendelea kulinda,”alisema Dk. Mwinyi.

Alisema miili ya wanajeshi hao inatarajiwa kufanyiwa taratibu za maziko keshokutwa.

Wakati huo huo, ndege ya Umoja wa Mataifa   namba UNO-855  iliyokuwa imebeba miili ya askari hao, ilitua katika ardhi ya Tanzania   katika Uwanja wa Ndege uliopo Kambi ya Jeshi la Anga (Air wing), Ukonga, Dar es Salaam jana saa 11.22 jioni.

Kazi ya kuteremsha miiili ilifanywa na wanajeshi waliokuwa wamejipanga wanane wanane na jeneza la kwanza lenye mwili liliteremshwa saa 11:35 huku jeneza  la mwisho likishushwa saa 11:59 jioni.

Idadi kubwa ya askari waliokuwa uwanjani hapo, walikuwa na sura za simanzi   walipokuwa wakishuhudia tukio hilo la kuteremshwa  miili ya wenzao.

Majeneza hayo 14 ambayo yalikuwa na rangi ya fedha yakiwa yamefunikwa bendera ya Umoja wa Mataifa, yaliingizwa kwenye magari saba yaliyoandikwa UN ubavuni mbele na nyuma yakiwa na namba na JWTZ.

Kila gari yalikaa majeneza mawili mawili na yalipelekwa katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo ambako yatahifadhiwa na kufanyiwa uchunguzi.

Novemba 8, mwaka huu, wanajeshi hao 14 waliuawa baada ya kambi yao ya Semuliki iliyopo Beni, Mkoa wa Kivu Kaskazini mashariki mwa DRC kuvamiwa na waasi.

Msafara huo uliokuwa na miili ya wanajeshi hao uliwasili Lugalo saa 12:35 jioni na kupelekwa moja kwa moja katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Lugalo.

Kazi ya kushusha miili hiyo ilianza muda huo na kukamilika saa 1:10 usiku.

Miili hiyo imehifadhiwa katika chumba hicho mpaka shughuli ya kuagwa itakapofanyika na kusafirishwa kwa ajili ya maziko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles