BADI MCHOMOLO NA MITANDAO
BAADA ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi, akili ya watu wengi kwa sasa ipo kwenye michuano mbalimbali ya Ligi Kuu Duniani.
Wakati nchi mbalimbali zikiendelea kufuatilia Ligi Kuu na michuano mbalimbali, Qatar wao wapo bize wakifanya maandalizi ya michuano hiyo ya Kombe la Dunia kwa ajili ya kivumbi hicho mwaka 2022.
Lengo kubwa la Qatar ni kuhakikisha wanaweka historia mpya ya Kombe la Dunia, ili wawe wakwanza kwa kupata sifa kubwa ya maandalizi ya michuano hiyo, kuanzia sehemu za kufikia wageni, sehemu za kupumzika, starehe, usafiri, viwanja vya michezo na mambo mengine mengi.
Tayari Qatar wameanza kuonesha maendeleo yao hasa katika suala la viwanja ambavyo vitatumika kwa ajili ya michuano hiyo.
SPOTIKIKI leo imekuanikia viwanja nane ambavyo vimetajwa kwa ajili ya kutumika kwenye michuano hiyo ifikapo 2022. Kwa mara ya kwanza michuano hiyo inatarajiwa kuanza kufanyika Novemba 21 na kumalizika Desemba 18.
Kawaida michuano hiyo imekuwa ikifanyika Juni hadi Julai mara baada ya kumalizika kwa michuano mbalimbali ya Ligi duniani, lakini itakuwa tofauti na Kombe la Dunia ambalo litafanyika Qatar.
Viwanja hivyo vyote, inadaiwa kuwa vipo umbali wa Kilometa 21 kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, Doha. Japokuwa vipo mbali kutoka Doha, lakini usafiri wa kutumia treni umeimarishwa kwa kiasi kikubwa, hivyo kutakuwa na uwezo wa kuangalia michezo miwili kwa siku kutokana na urahisi wa usafiri huo.
Al Wakrah
Huu ni uwanja ambao utachukua idadi ya watazamaji 40,000. Upo umbali wa Miles 14 kutoka mjini Doha.
Sifa ya uwanja huo ni kwamba umefunikwa sehemu kubwa ya juu, lakini imeachwa nafasi ambayo kuna wakati inafunikwa kama kutakuwa na jua kali na kuna wakati inaachwa wazi.
Ndani ya uwanja huo kuna mfumo umewekwa kwa ajili ya wakati ya jua mashabiki kupigwa na ubaridi na wakati wa ubaridi mashabiki kupigwa na joto la kawaida, hivyo uwanja huo unatumika wakati wowote ndani ya mwaka.
Al Bayt – Al Khor City
Huo ni uwanja ambao utakuwa unachukua jumla ya watazamaji 60,000, upo umbali wa miles 27 kutoka mji wa Doha. Hicho ni kiwanja cha pili kwa ukubwa nchini humo kwa ajili ya Kombe la Dunia.
Uwanja huo utatumika kwa michezo yote kuanzia nusu fainali. Uwanja huo umewekewa mfumo wa kupoza joto kwa kuwa wanaamini wakati huo wa michuano joto litakuwa linafikia nyuzi 30. Kuna wakati joto likiwa kali uwanja unafunikwa hadi juu na kuanza kutumia mfumo wa AC.
Al Rayyan
Huu ni uwanja ambao utakuwa unachukua jumla ya watazamaji 40,000. Upo umbali wa mile 14 kutoka mji wa Doha. Uwanja huo utakuwa unatumika kuanzia mwanzo wa michuano hadi hatua ya robo fainali.
Education City
Kutakuwa na jumla ya viti vya watazamaji 40,000. Uwanja huo upo umbali wa mile 7 kutoka Doah mjini. Lengo la uwanja huo ni kuwa uwanja wa timu ya taifa ya wanawake mara baada ya kumalizika kwa michuano hiyo ya Kombe la Dunia.
Uwanja huo umetengenezwa na utakuwa na muonekano kama madini ya Diamond ‘Almasi’ kwa muonekano wa nje, hivyo uwanja huo unaweza kuuita Diamond au Education.
Al Thumama
Uwanja huu upo umbali wa mile 8 kutoka mji wa Doha, unatengenezwa kwa ajili ya kuchukua watazamaji 40,000. Huo utakuwa uwanja wa kwanza wa Kombe la Dunia nchini humo ambao ramani yake imetengenezwa na mtu wa hapo nchini Qatar ambaye anajulikana kwa jina la Ibrahim Al Jaidah.
Asilimia 80 ya nje ya uwanja huo kuna viwanja vingine mbalimbali vya kisasa kwa ajili ya kufanyia mazoezi, lakini viwanja hivyo vipo wazi havijajengewa.
Ras Abu Aboud
Upo umbali wa mile 6 kutoka Doha mjini. Utakuwa unachukua jumla ya watazamaji 40,000. Huu ni uwanja wa kipekee na umetengenezwa kwa kutumia makontena 998 pamoja na vifaa vingine na uwanja huo unadaiwa kwamba ni rahisi kuubomoa mara baada ya kumalizika kwa michuano hiyo ya Kombe la Dunia.
Uwanja huo upo pembezoni mwa bahari ya Doha Corniche na utatumika hadi hatua ya nusu fainali. Waliamua kutumia makontena kwa ajili ya kupunguza gharama za vifaa.
Lusail
Huu ni uwanja mkubwa kuliko yote ambayo itatumika kwenye michuano hiyo ya Kombe la Dunia. Utakuwa unachukua jumla ya watazamaji 80,000, upo umbali wa mile 10 kutoka Doha mjini.
Uwanja huo utatumika kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa ufunguzi, mchezo wa fainali pamoja na michezo mingine muhimu ambayo itachaguliwa.
Khalifa International
Huu upo umbali wa mile 8 kutoka Doha mjini, unatengenezwa kwa ajili ya kuchukua watazamaji 40,000. Uwanja huo ulikuwa unatumika kama uwanja wa taifa kwa kipindi cha nyuma, lakini kuelekea michuano ya Kombe la Dunia wameamua kuurekebisha tena.
Awali ulifunguliwa tangu mwaka 1979. Mwaka 2009 timu ya taifa ya Brazil iliwahi kucheza mchezo wa kirafiki kwenye uwanja huo dhidi ya England.