26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Drinkwater shujaa wa Leicester, hana nafasi Stamford Bridge

NA BADI MCHOMOLO



UKITAJA majina 11 ya wachezaji nyota ambao waliandika historia katika msimu wa 2015-2016 kwenye michuano ya Ligi Kuu nchini England, hauwezi kuliacha jina la Danny Drinkwater, raia wa nchini England.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28, alitoa mchango mkubwa katika safu ya kiungo ya timu ya Leicester City na kuisaidia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu na kuandika historia mpya. Leicester City ni klabu ambayo ilimjenga na kufahamika kwa kiasi kikubwa kuliko klabu zingine zaidi ya nne ambazo alipita kwa mkopo akitokea Manchester United.

Alianza kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Manchester United tangu mwaka 2008 hadi 2012, lakini kwa kipindi hicho chote hakuweza kupata namba kwenye kikosi cha kwanza hadi anaondoka kwa mkopo na kujiunga na klabu ya Huddersfield Town, Cardiff City, Watford na Barnsley kabla ya 2012 kujiunga na Leicester City.

Msimu wa 2016, alitajwa kuwa miongoni mwa viungo bora ndani ya Leicester City, huku akiwa na ushirikiano mkubwa na N’Golo Kante, hivyo ubora wake uliifanya Leicester kuwa mabingwa.

Kutokana na ubora huo, Kante baada ya kumalizika kwa msimu huo alijiunga moja kwa moja na Chelsea na akafanikiwa tena kutwaa taji hilo akiwa na Chelsea, lakini bado Chelsea waliamini kuwa Kante anaweza kufanya kazi vizuri akiwa anacheza pamoja na Drinkwater.

Msimu uliofuata uongozi wa klabu hiyo ukakaa mezani na Drinkwater na hatimaye kuweza kuinasa saini yake huku wakiamini safu yao ya kiungo itakuwa bora zaidi baada ya mabingwa hao kuwa pamoja.

Drinkwater alijiunga na klabu hiyo kwa uhamisho wa kitita cha pauni milioni 35, ambazo ni zaidi ya bilioni 102 za Kitanzania kwa mkataba wa miaka mitatu na nusu na anachukua pauni 90,000 kwa wiki zaidi ya milioni 264.

Kwa sasa mchezaji huyo anaonekana kuwa anachukua mshahara wa bure kutokana na kukosa nafasi ya kudumu ndani ya kikosi cha kwanza, mbali na ushindani uliopo, lakini kocha wa timu hiyo Maurizio Sarri ameweka wazi kuwa, mchezaji huyo hafiti kwenye mifumo yake ni bora atafute timu nyingine.

Mara ya mwisho kwa mchezaji huyo kuonekana akiwa na jezi ya Chelsea ilikuwa Machi mwaka huu, tangu hapo hadi sasa anaonekana akiwa na jezi hiyo wakati wa mazoezi, lakini anaweza kuonekana tena ameivaa wakati yupo benchi.

Amekosa nafasi kwenye michezo mingi sana jambo ambalo linaweza kumfanya kiwango chake kushuka kwa kuwa anakosa uzoefu wa michezo mbalimbali. Baada ya kufanya vizuri akiwa na Leicester City, mchezaji huyo aliitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha timu ya taifa England mwaka jana, hadi sasa amecheza jumla ya michezo mitatu.

Tangu ameondoka Leicester City mwaka jana hadi sasa mchezaji huyo amepata nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza mara tano tu huku akiwa amecheza jumla ya michezo 12 ya Ligi Kuu na kufunga bao 1.

Kwa upande mwingine unaweza kusema kuwa, mchezaji huyo alikuwa na haraka sana ya kuondoka ndani ya Leicester City, alitakiwa kuwa mvumilivu ili aweze kujitengenezea jina kwa misimu kadhaa kabla ya kwenda kujiunga na klabu zingine kubwa.

Ni wazi kwamba kila mchezaji ana ndoto za kuja kucheza klabu kubwa duniani, hivyo mchezaji huyo baada ya Chelsea kuweka ofa hakuona sababu ya kusubiri, lakini kwa sasa anakosa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

Wachezaji wengine ambao walifanya vizuri wakiwa na Leicester City ni pamoja na Jamie Vardy. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 hadi sasa hajawahi kucheza soka katika klabu kubwa zaidi ya Leicester City.

Alikuwa mmoja wa wapachikaji mabao ndani ya Leicester City wakati wanatwaa ubingwa, kulikuwa na ofa mbalimbali kutoka kwa klabu kubwa Ulaya, lakini mchezaji huyo hakuweza kuondoka akaamua kuendelea kuwa staa wa timu hiyo.

Kukaa kwake ndani ya Leicester City kulikuwa na maana kubwa, aliamini kuwa, kuna wachezaji wengi wataondoka, hivyo atakuwa mchezaji wao tegemeo katika kikosi hicho na ndivyo ilivyo hadi sasa badala ya wachezaji wengine kuondoka kama vile Riyad Mahrez.

Mahrez kutokana na uwezo wake, alipata nafasi ya kujiunga na klabu ya mabingwa wa soka nchini England msimu uliopita, Manchester City na anapata nafasi ya kucheza huku akiwa amecheza jumla ya michezo 11 ya Ligi Kuu msimu huu na kupachika mabao manne.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles