Na Gustafu Haule, Pwani
Wakala wa barabara (Tanroads) mkoa wa Pwani unahitaji jumla ya Sh bilioni 57.187 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi wanaopitiwa na miradi ya utengenezaji wa barabara .
Meneja wa Tanroads mkoani Pwani, Mhandisi Yudas Msangi ametoa taarifa hiyo leo Desemba 22, katika kikao cha bodi ya barabara kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu Mkoa wa Pwani iliyopo Kibaha.
Msangi amesema miradi mingi inakwama kuendelea kutokana na changamoto ya ukosefu wa fedha za barabara kwahiyo lazima tuwe wavumilivu mpaka hapo fedha zinapopatikana.
Amesema Mkoa wa Pwani ipo miradi mingi ya barabara imefanyiwa usanifu na inakwama kutokana na ukosefu wa fedha za fidia lakini hata hivyo wanaendelea kufuatilia ili kuona namna ya kuendelea na utengenezaji wa barabara hizo.
Amewaomba wabunge kuendelea kushirikiana kwa kuhakikisha wanakwenda kuisemea bungeni changamoto hiyo ili hiweze kupata majibu ya haraka na hivyo kutekeleza miradi hiyo.
Majibu ya meneje huyo yamekuja baada ya baadhi ya wabunge akiwemo, Michael Mwakamo wa Kibaha Vijijini kuhoji juu ya ujenzi wa barabara ya Makofia- Mlandizi -Ruvstation mpaka Mzenga ambayo iliahidiwa na Rais kujengwa kwa kiwango cha lami.
“Barabara ya Mlandizi -Ruvustesheni, Mzenga iliahidiwa na Rais kuwekwa lami na hata mwaka jana kabla ya kampeni alipita Mlandizi na kusisitiza kujenga kwa lami barabara hiyo,sasa je ni hatua gani imefikia? alihoji Mwakamo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo ambaye ni mwenyekiti wa bodi hiyo amesema ni vyema Tarura na Tanroads waonyeshe jumla ya miradi kwa kila halmashauri na waonyeshe mgawanyo wake.
Amesema akishapata jedwali hilo litakuwa limetoa ufafanuzi wa kutosha wa namna ya kutekekeleza miradi na hata kama fedha zinakuja kidogo itaangaliwa namna ya fedha hizo kugawanya kwa ulinganifu ili kusiwe na upendeleo wa eneo fulani.