MOSCOW, URUSI
RAIS wa nchini Urusi, Vladimir Putin, amewataka wakandarasi wa viwanja vya michezo kuongeza kasi na kukamilika kwa muda uliopangwa kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Dunia 2018.
Rais huyo amedai kwamba kuna dalili za ucheleweshwaji wa kumaliza ujenzi huo, hivyo wakandarasi hao wakishindwa kufanya kazi kama walivyokubaliana watachukuliwa hatua.
Viwanja hivyo vinajengwa kwenye mji wa St. Petersburg, ambapo walitenga eneo maalumu kwa ajili ya ujenzi wa viwanja hivyo, likijulikana kwa jina la Zenit Arena.
Putin amewataka wahusika wenyewe kujitahidi kuumaliza uwanja ambao utatumika kwa michezo mingi ya fainali hizo pamoja na kutumika katika hatua ya nusu fainali.
“Hakuna sababu ya kuchelewa kwa ujenzi wa viwanja vyote ambavyo vimekusudiwa kujengwa.
“Tulikubaliana muda wa kumaliza, lakini itashangaza kuona hadi muda ambao umekusudiwa viwanja hivyo havijakamilika.
“Wakandarasi wanatakiwa kuhakikisha wanamaliza kama muda ulivyopangwa, kinyume na hapo wanatakiwa kuchukuliwa hatua,” alisema Putin.
Msemaji wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Delia Fisher, ameweka wazi kwamba waratibu wa michuano hiyo ya Kombe la Dunia wanatarajia kukabidhiwa viwanja hivyo Desemba mwaka huu kwa ajili ya kuvikagua.