23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Pumzika kwa amani Samweli Sitta, vijana tunakulilia

samuel-sitta

NILIPOSIKIA taarifa za kifo cha aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samweli Sitta nilishtuka sana. Hazikuwa taarifa nzuri kwa hakika.

Lakini bado ukweli utabaki palepale kwamba, mzee wetu Sitta, Spika mwenye msimamo kupata kutokea katika nchi yetu ametangulia mbele za haki.

Sitta, ambaye alipenda kujulikana kama mzee wa kasi na viwango ameondoka na hatutamuona tena. Nakumbuka mengi kuhusu mzee wetu huyu.

Ana mchango mkubwa katika Serikali yetu hasa kutokana na nafasi yake ya Uspika aliyoitumikia katika kipindi cha miaka mitano (2005 – 2010) na hata baadaye alipoteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba mwaka 2014.

Mzee Sitta, ambaye alipata kuwa mbunge wa Jimbo la Urambo na baadaye Urambo Mashariki baada ya kugawanywa, kuanzia mwaka 1975 hadi 2015 kwa vipindi tofauti, amepata kushika nafasi mbalimbali ikiwemo ya Waziri wa Katiba na Sheria katika Serikali ya Awamu ya Pili, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi.

Baadaye mwaka 2010 aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Waziri wa Afrika Mashariki na baadaye akahamishiwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi.

Kiukweli amefanya kazi kubwa sana, lakini sisi hapa Swaggaz, kama watu wa burudani tunamkumbuka mzee wetu Sitta kwa kujitoa kwake kuwa karibu na vijana, kuwasaidia kukua kisiasa na kutowabeza.

Wanasiasa wengi machachari vijana, walipata kupitia katika mikono ya mzee Sitta.

Kupitia andiko lake mwenyewe, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Zubeir Kabwe, anakubali kukuzwa kisiasa na mzee Sitta. Zitto anamtaja mzee Sitta kama kiongozi wa mfano aliyepata kujifunza siasa safi kupitia kwake.

Katika kipindi cha uongozi wake wa Uspika, ndipo vijana machachari walipopewa nafasi na kuibuka bungeni zaidi kuliko kipindi kingine chochote.

Mzee Sitta aliamini katika kuwekeza kwa vijana. Aliwatunza kisiasa na kuwapa miongozo ambayo kwa hakika imewanyoosha na wengine kupata nafasi kubwa hivi sasa serikalini.

Nje ya kuwa karibu na vijana, mzee wetu Sitta alikuwa karibu na burudani. Alipenda burudani na kusaidia vikundi mbalimbali vya uimbaji.

Mfano mzuri ni namna alivyojitoa kanisani kwake, KKKT – Kinondoni kwa vijana na kwaya nyingine kanisani hapo. Hiyo yote ni kutokana na mapenzi yake na burudani lakini pia kusaidia kazi ya Mungu iendelee mbele.

Pole nyingi kwa mama yetu, Magreth Sitta (Mbunge wa Urambo Mashariki), watoto wake, Bunge na Serikali kwa ujumla pamoja na ndugu, jamaa na marafiki kwa msiba huu mzito kwa Taifa letu.

Kazi ya Mungu haina makosa, upumzike kwa amani baba yetu mpendwa, Samweli Sitta.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles