25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Bugando yaanza upimaji wa ugonjwa wa moyo

bugando-hospital-close-up

Na CLARA MATIMO-MWANZA

WATOTO 35 kati ya 50 waliofanyiwa  uchunguzi wa ugonjwa wa moyo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) kuanzia  Novemba 7 hadi 10 mwaka huu kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo wamekutwa na ugonjwa huo.

Akizungumza jana hospitalini hapo na waandishi wa habari, Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji wa Moyo na vifua wa BMC, Profesa William Mahalu, alisema watoto hao wamebainika kuwa na tatizo la moyo baada ya uchunguzi kufanywa na timu ya madaktari bingwa wa moyo kutoka Madras Medical Mission Chennai wa nchini India, iliyowasili hospitalini hapo tangu Novemba 7, mwaka huu, kwa ajili ya kutoa matibabu ya uchunguzi na upasuaji wa moyo kwa wagonjwa hadi Novemba 13, mwaka huu.

Alisema kutokana na uchunguzi huo, wanatarajia kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto zaidi ya 10 na watu wazima wanne kwa kushirikiana na timu ya wataalamu hao, hivyo alichukua nafasi hiyo kumpongeza Dk. Glory Joseph, ambaye alikuwa nchini India kwa ajili ya masomo, aliyefanikisha kuwaleta wataalamu hao.

“Pamoja na upasuaji, jambo jema ni kwamba wenzetu hawa wakiondoka wanatuachia vifaa vyao ambavyo wamekuja navyo, hivyo vitatusaidia kuendelea kutoa huduma hizi kwa wagonjwa wetu hata wakiondoka, hili ni jambo la kujivunia zaidi,” alisema Prof. Mahalu.

Naye Dk. Glory Joseph, ambaye ndiye mratibu wa safari ya wataalamu hao kutoka nchini India, alisema aliamua kuwaomba kuja nchini baada ya kuona kila mwaka Serikali inatumia gharama kubwa kugharamia matibabu ya wagonjwa wa moyo nchini India ambapo mgonjwa mmoja hugharimu Sh milioni 25.

“Kipindi chote nilichokuwa nchini India nimeshuhudia Serikali ikileta wagonjwa 50 kwa ajili ya matibabu kila mwaka, kwa kweli niliumia sana, nilipopiga hesabu nikaona gharama ya kuwasafirisha hawa taalamu ni Sh milioni 6 kila mmoja, ambayo inakuwa imejumuisha na vifaa vyao vya matibabu, ndipo nikaenda kuwaomba ili waje kutoa matibabu huku, wakakubali  tukaanza harakati za kutafuta wafadhili, namshukuru Mungu azma yangu imefanikiwa,” alisema.

Alisema timu hiyo imejumuisha madaktari bingwa wa moyo wanane, wauguzi wanne na wataalamu wa dawa za usingizi wawili, ambao watatoa huduma ya matibabu na upasuaji BMC na wakitoka hapo Novemba 17 na 18 watakuwa katika Hospitali ya Tumaini, iliyoko mkoani Dodoma, kwa ajili ya kutoa matibabu ya ugonjwa huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles