NA HARRIETH MANDARI-DAR ES SALAAM
NI ukweli usiopingika kwamba nchini Tanzania waajiriwa wapya walio wengi hukutana na changamoto mbalimbali, ikiwamo kumudu gharama za kuanzia maisha pale wanapopata ajira.
Kwa kuzingatia hilo, Mfuko wa Pensheni wa PSPF umeanzisha huduma mpya ya utoaji mkopo kwa waajiriwa hao ili kuwawezesha kujiandaa vyema kukabiliana na changamoto hizo.
Mfuko huo kwa kushirIkiana na Benki ya CRDB unalenga kupanua wigo wa huduma na fursa kwa wanachama wote wa PSPF ambapo wanachama watapata mkopo kwa riba nafuu kwa kiwango ambacho ni chini ya kile kilichotolewa katika taasisi nyingine za kifedha nchini.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa PSPF, Adam Mayingu, alisema mikopo hiyo ni pamoja na mkopo wa elimu (Education Scheme), mkopo wa kuanzia maisha (startup life loan scheme) na mkopo wa viwanja (Nipo site na PSPF).
“Mpango huu wa kutoa mikopo kwa wanachama tuliuanza tangu Desemba mwaka 2014 kwa kupitia taasisi nyingine ya fedha ambapo mfuko huu ndio wa kwanza kuingiza sokoni huduma hii muhimu kwa wanachama wake wa viwanja, nyumba, wa kuanzia maisha na pia mkopo kwa wastaafu,” alisema Mayingu.
Akaongeza kuwa kwa upande wa mkopo wa elimu, mwanachama anaweza kukopa kwa ajili ya kujiendeleza kielimu katika ngazi yoyote ile mfano stashahada, shahada ya uzamili na hata mafunzo ya ufundi.
Vilevile alifafanua kuwa kwa upande wa mkopo wa kuanzia maisha, mwanachama aliyepata ajira kwa mara ya kwanza huwa ana mahitaji yake muhimu ambapo ataweza kukopa mishahara yake ya miezi miwili na hivyo kuweza kujipanga kwa maisha mapya ya ajira.
Mayingu alisema lengo kubwa la mfuko huo pia ni kuhakikisha Mtanzania anatimiza ndoto yake ikiwa ni katika masomo kwa kupitia huduma hizo mpya.
“Mara zote PSPF inajivunia ubunifu ambao umefanya mfuko huu kuwa wa kwanza hasa kwa upande wa mafao kwa wanachama na ubunifu huu si tu kwa wanachama wake, bali hata kwa mifuko mingine ya pensheni nchini,” alisema.
Mfuko wa PSPF ni wa kwanza nchini kuanzisha mkopo wa kuanzia maisha kwa waajiriwa wapya miongoni mwa mifuko ya pensheni nchini na ni anzilishi katika kutoa mikopo ya nyumba na ule wa viwanja kwa wananchama wake.
Kwa upande wa mkopo wa viwanja, mwanachama wa PSPF aliyechangia mfuko kwa kipindi cha miezi sita na umri usiozidi miaka 60 anaweza kukopa mkopo huo kupitia Benki ya CRDB na kurejesha kupitia makato madogo madogo ya mshahara wake kati ya miaka miwili hadi mitano.
Katika awamu ya pili ya utekelezaji wa huduma hiyo, yapo maeneo yaliyolengwa katika mpango ambayo ni pamoja na mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Songea, Tabora, Lindi, Singida, Arusha, Bukoba, Mwanza, Iringa, Shinyanga, Mpanda, Katavi, Kigoma na Mtwara.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Charles Kimei, alisema baada ya Mfuko wa PSPF kuainisha aina za changamoto ambazo Watanzania wengi waliostaafu wamekuwa wakikumbwa nazo, ndipo kulionekana umuhimu wa kuanzisha huduma hizo mpya kwa nia ya kuwatatulia matatizo wateja.
“Azma yetu ni kuhakikisha kuwa kwa ushirikiano na wadau wetu, tunamkomboa kiuchumi mwananchi hususan mwenye kipato cha chini kwa kumpatia mkopo wenye riba nafuu kiasi cha asilimia 14 tu kwa mwaka, ikujumuisha bima ya maisha ili endapo atafariki familia yake isaidiwe,” anasema Kimei.
Akaongeza kuwa mikopo hiyo yote itatolewa kwa haraka bila mlolongo mrefu kwa kuwa inadhaminiwa na Mfuko wa PSPF na marejejsho yake ni kuanzia mwaka mmoja hadi mitano.
Alisema ushirikiano baina ya CRDB na Mfuko wa PSPF una mwendelezo mpana ambapo kwa pamoja wamedhamiria muda si mrefu kuingiza sokoni huduma mpya ya mkopo kwa ajili ya wastaafu (Pensioners).
“Mpango huu wa utoaji mikopo kwa wastaafu una lengo la kuleta faraja na kuwasaidia wastaafu katika kukidhi mahitaji yao mbalimbali kimaisha ikiwamo kulipia gharama za matibabu, ada za shule za watoto au wajukuu zao au hata kuendesha biashara ndogondogo zitakazosaidia kupunguza ukali wa maisha ya kila siku,” alisema.
Akaongeza kuwa kwa huduma hiyo, wataweza kujenga mazingira mazuri kwa wastaafu walio wanachama wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF ili kustaafu kusiogopwe na kuonekana ni mwanzo wa kuanza kipindi cha maisha ya shida yasiyo na matumaini.
“Tunataka wafanyakazi wetu wanapopata barua za kustaafu wasihuzunike kama ilivyozoeleka katika jamii ya Kitanzania,” aliongeza.
Mfuko wa Pensheni wa PSPF ni Hifadhi ya jamii iliyoanzishwa na Sheria ya Mafao ya Hitimisho la Kazi kwa Watumishi wa Umma namba 2 ya mwaka 1999, sura ya 371 nchini Tanzania.
Mfuko huo unatoa huduma za hifadhi ya jamii kwa mfumo wa lazima na wa hiari, vilevile unahudumia wanachama na wategemezi zaidi ya 467,685 kutoka sekta mbalimbali nchini.
Aina ya wanachama wa mfuko wa PSPF ni watumishi wa umma na watu wote hiari walio katika sekta isiyo rasmi.