25.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

PSG kumpiga faini Neymar Ml. 972

PARIS, UFARANSA

UONGOZI wa mabingwa wa Ligi Kuu nchini Ufaransa, PSG, unaripotiwa kuwa kwenye mipango ya kutaka kumpiga faini mshambuliaji wao Neymar de Santos kitita cha pauni 340,000, ambazo ni zaidi ya milioni 972 za Kitanzania kutokana na kuchelewa kuripoti kambini.

Wachezaji wa timu hiyo walitakiwa kuripoti mapema wiki hii na tayari wengi wao wamewasili jijini Paris kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi, lakini Neymar raia wa nchini Brazil hadi sasa hajawasili na hakuna taarifa yoyote alioitoa juu ya kuchelewa kwake.

Kwa mujibu wa gazeti la Marca la nchini Hispania, mchezaji huyo atakatwa bonasi yake ya pauni 340,000 ambayo alitakiwa kuchukua Julai kwa sababu hadi sasa hajajiunga na mabingwa hao.

Fedha hizo ambazo atakatwa Neymar, moja kwa moja zitaingia kwenye mfuko wa timu hiyo wa kusaidia mambo mbalimbali ya maendeleo ya soka.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27, amekuwa akionekana nyumbani kwao nchini Brazil hasa katika michuano ya Copa America ambayo imemalizika wiki iliopita kwa Brazil kushinda mabao 3-1 dhidi ya Peru, lakini Neymar hakucheza hata mchezo mmoja kutokana na kusumbuliwa na majeruhi wakati wa maandalizi ya michauno hiyo.

Neymar alijiunga na PSG mwaka 2017 akitokea kwa mabingwa wa Ligi Kuu nchini Hispania, Barcelona kwa uhamisho wa kitita cha pauni milioni 198 na kuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha katika historia ya soka.

Hata hivyo, kwa sasa mchezaji huyo anaonekana kuwa na uhusiano mbaya na uongozi wa timu yake ya PSG na kufikia hatua ya kutangaza kuwa anataka kuondoka wakati huu wa uhamisho wa wachezaji.

Mchezaji huyo anahusishwa kutaka kurudi katika klabu yake ya zamani ya Barcelona, lakini awali kulikuwa na taarifa kwamba anaweza kwenda kujiunga na kikosi cha kocha Zinedine Zidane, Real Madrid.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles