24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 19, 2024

Contact us: [email protected]

Project Echo Tanzania kutoa mafunzo zaidi kwa wataalamu wa afya nchini

Na Rose Joseph, Dodoma

Kamati Tendaji ya “Project ECHO” Tanzania, iliyo chini ya Wizara ya Afya, imekutana Dodoma leo katika kikao chake cha 12 cha mwaka kilichofanyika katika Hoteli ya Morena na kuwakutanisha wadau mbalimbali katika Sekta ya Afya wakiwemo wataalamu kutoka TAMISEMI, Wizara ya Afya, Wataalamu wa Maabara, wadau wa maendeleo katika sekta ya afya na wataalam kutoka mabaraza ya wataam (Professional councils), Chuo kikuu Mzumbe na wafadhili wa Mradi (CDC).

Wajumbe wa Mkutano wa Kamati Tendaji ya Project ECHO Tanzania, wakiwa katika picha ya Pamoja baada ya kuhitimisha kikao. Walioketi katikati ni Mwenyekiti wa kikao, Mary Mtui, kulia kwako ni Dk. Mackfallen Anasel wa Chuo Kikuu Mzumbe na kushoto kwake ni Dk. Paul Chaote, kutoka TAMISEMI.

Kikao hicho kilifunguliwa na Mwenyekiti wa muda wa Kikao hicho, Mary Mtui, Msajili wa Baraza la Wataalamu wa Maabara kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali.  

Amesema, pamoja na mambo mengine kikao hicho, kimekusudia kujadili na kuweka mikakati ya namna ya kuongeza ushiriki wa wataalamu wa Afya katika mafunzo kwa njia ya mtandao “ECHO Platforms” pamoja na namna wataalamu wa afya wanavyoweza kupanda madaraja/vyeo kwa kushiriki kwenye mafunzo hayo ambayo yanatolewa kila wiki kupitia vituo 9 (hubs) na watoa huduma za afya kutoka katika vituo (Spokes) zaidi ya 349 vilivyofungiwa vifaa vya mafunzo nchi nzima wananufaika na mafunzo hayo.

Miongoni mwa mafunzo yanayotolewa kwa sasa ni pamoja na kliniki za “Adult HIV, Pediatric HIV, MDR TB, HVL, HIV LAB, Supply Chain na AMS/IPC ECHO”.

Hadi kikao cha 12 cha mwaka cha Kamati ya Utendaji, inakadiriwa zaidi ya CPD pointi 1,000 zimetolewa kwa watumishi wa afya ambao wamekuwa wakipata mafunzo kwa njia hiyo ya mtandao, huku zaidi ya watumishi na watoa huduma za afya 650 wakishiriki mafunzo nchini nzima kila wiki.

Kikao hicho kimeweka mikakati mingi ya kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wa afya popote walipo kwa kupata mafunzo ya kina yatakayosaidia kuboresha huduma za afya katika vituo vyote vya Afya nchini, pamoja na kuongeza wigo wa mafunzo kwa kutumia vifaa vya kisasa kwa kushirikiana na wafadhili, ili uwekezaji huo uweze kuwa na tija katika utoaji huduma za afya kwa wananchi.

Wakichangia mkutano huo, wadau wamepongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya na Wadau wa maendeleo CDC kwa kuwekeza katika mfumo wa mafunzo kwa njia ya mtandao; na hivyo kuwajengea uwezo wataalamu wa Afya wakiwa mahali pa kazi.

Akieleza mikakati zaidi ya Wizara; Mratibu wa Project ECHO Tanzania Bw. Jacob Lusekelo amesema, Wizara inakusudia kupanua wigo wa mafunzo na usimamizi kwa kuanzisha “Super Hub” nchini ambayo itakuwa na uwanda mpana zaidi wa kutoa mafunzo, mwongozo na usimamizi kwa wataalamu wa huduma za afya (immersion training).

Kikao hicho cha siku moja kimehudhuriwa na mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Huduma za Afya (TAMISEMI), pamoja na viongozi wengine kutoka Wizara ya Afya, TAMISEMI, wawakilishi kutoka Mabaraza ya Kitaaluma Tanzania, Chuo Kikuu Mzumbe, MDH, THPS, MNH na NBTS.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles