24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

PROFESA NDULU AAGA KWA UJUMBE MZITO

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


“HUYU ndiye mrithi wangu.” Ni maneno ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, alipokuwa akimtambulisha gavana mteule, Profesa Florens Luoga.

Hayo aliyasema jana Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Pili wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha kwa mwaka 2018/22.

Alisema pamoja na matokeo ya tathmini iliyofanyika, yanaonyesha kwamba wananchi walio karibu na huduma za fedha wameongezeka kufikia asilimia 86 ya Watanzania (watu wazima) mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 29 ya mwaka 2012.

Profesa Ndulu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za Fedha, anayemaliza muda wake, alisema Watanzania wanaotumia huduma za kifedha hasa kupitia asasi za kifedha na mitandao ya simu, wameongezeka kutoka asilimia 17 mwaka 2009 hadi 11 mwaka 2006, na hadi sasa (2017) takwimu zinaonyesha kwamba wananchi asilimia 65 wanatumia huduma hizo nchini.

“Huyu ndiye mrithi wangu (Profesa Luoga), mtakuwa naye katika majukumu haya muda mchache ujao. Hata hivyo, kutokana na mafanikio haya makubwa, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika na ya sita duniani kwa kuweka mazingira bora ya utoaji na upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi,” alisema Profesa Ndulu katika mkutano huo uliohudhuriwa na wadau na watoa huduma za fedha nchini kutoka taasisi mbalimbali.

Kwa upande wake, aliyekuwa mgeni rasmi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alimshukuru Profesa Ndulu kwa kazi kubwa aliyoifanya kupitia Benki Kuu.

Alisema uwepo wa uchumi imara na unaokua kwa kasi, ni miongoni mwa vigezo vinavyochangia ukuaji wa haraka wa sekta ya fedha nchini.

Majaliwa alisema uwepo wa miundombinu muhimu iliyojengwa na inayojengwa na Serikali na sekta binafsi katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya vijijini na ongezeko la watumiaji wa mitandao ya simu na huduma za mawasiliano, ni kati ya fursa nzuri iliyotajwa kwenye mpango huo.

“Kati ya fursa nzuri iliyotajwa kwenye mpango huo, ni uwepo wa uchumi imara na unaokua kwa kasi. Tukijenga vizuri juu ya misingi hii, tunaweza kupiga haraka hatua za maendeleo katika sekta ya fedha na uchumi kwa ujumla wake,” alisema.

Alisema ameupitia mpango huo na kubaini kuwa umeainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi hii katika harakati zake za kuongeza matumizi ya huduma za kifedha.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alikiri kuwa mpango huo umeainisha fursa ambazo zinaweza kutumika ili kukabiliana na changamoto hizo na hatimaye kuongeza matumizi ya huduma za kifedha.

“Changamoto zilizoainishwa ni pamoja na kuimarisha utawala wa matumizi ya fedha taslimu kwa ajili ya malipo badala ya matumizi ya mifumo ya kielektroniki ya malipo na kukosekana kwa utambulisho wa kipekee (unique identification) kwa Watanzania walio wengi.

“Uhalifu kwa njia za mtandao (cyber-crime); kukosekana kwa mifumo madhubuti ya taarifa za kutosha za watumiaji wa huduma za fedha na dhamana zao; na uelewa mdogo wa masuala ya kifedha,” alisema Majaliwa.

Katika hatua nyingine, alisema wataalamu wa uchumi duniani wanaeleza kwamba jamii ambayo imejijengea utamaduni wa kujiwekea akiba katika asasi za kifedha, ina fursa kubwa ya kupata maendeleo endelevu na ya haraka.

“Hii ni kwa sababu uwekaji akiba ndiyo kiini na nguzo ya uwekezaji wa miradi ya maendeleo, na bila uwekezaji wa miradi ya maendeleo, hakuna maendeleo. Nchi zote zilizoendelea zimejijengea utamaduni huu wa wananchi.

“Taarifa ya Mpango wa Pili wa Huduma Jumuishi za Kifedha inaonyesha kuwa asilimia kubwa ya Watanzania (watu wazima) wanamiliki simu za mkononi na wanatumia simu hizo kufanya miamala ya kifedha. Kwa msingi huo, nashauri kuwepo kwa ushirikiano wa karibu baina ya wadau wa taasisi za fedha na wadau wa TEHAMA ili kuimarisha matumizi na mtandao wa kifedha vijijini ili iwe kichocheo cha uchumi,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabenki Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei, alimsifu Profesa Ndulu kwa kuwa mlezi wa mabenki nchini na katika kipindi chake cha uongozi, hakuna benki iliyokufa ila tatizo lilibaki kwa benki zenyewe.

Kutokana na hali hiyo, alisema wenye mabenki wana haja ya kubadili mtazamo na kujikita kwenye ngazi ya chini ambako kuna watumiaji wengi zaidi.

“Wenye kampuni za simu wameonyesha kuwa inawezekana kufikisha huduma kwa watu wa chini kupitia simu zao, nasi tukitumia vifaa hivyo, tunaweza kuwafikia wananchi wengi kwa kuwapa huduma zetu,” alisema.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles