23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU NINAISHI NA RISASI

Na NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM


MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amesema bado anaishi na risasi moja mwilini.

Lissu alishambuliwa kwa risasi Sepemba 7, mwaka huu akiwa nje ya makazi yake mjini Dodoma, muda mfupi baada ya kuhudhuria kikao cha Bunge.

Akizungumza katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha Azam jana akiwa hospitalini Nairobi nchini Kenya, Lissu alisema hali yake inaendelea vizuri ingawa hajapona kabisa.

“Bado niko hospitali na maana yake ni kwamba sijapona kabisa kwa sababu risasi 16 ziliingia mwilini mwangu, saba zilitolewa na madaktari na moja bado iko kwenye mwilini.

“Lakini, sina majeraha ya risasi, hali ni nzuri kuliko nilivyoletwa mwanzoni kwani nililetwa vipande vipande kabisa,” alisema Lissu.

Katika mahojiano hayo ya dakika zipatazo saba, Lissu alisema mkono wake wa kushoto haunyooki moja kwa moja kwa sababu kwenye kiwiko alipigwa risasi ikavunjavunja mifupa.

“Katika mkono wa kulia, madaktari wameuunga kwa kuweka chuma kinachounganisha mfupa.

“Kina mama cheza wananinyoosha, basi umefika wakati nikiwaona mahali, nawaogopa kabisa,” alisema mbunge huyo ambaye ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

 

ANALI-MISS BUNGE

Pamoja na hayo, Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alisema anapenda kazi ya ubunge, hivyo kitendo cha kulala wodini kwa miezi mitatu, kinamkosesha mambo mengi.

“Mimi napenda kazi ya ubunge, kuna watu wanapenda ubunge kwa sababu una fedha, manufaa, unaitwa mheshimiwa na hukai kwenye foleni, lakini mimi napenda yale mapambano ya mle ndani (bungeni).

“Mule bungeni unamkaba waziri mpaka anakosa pa kukimbilia, hiyo ndiyo kazi ninayoipenda. Kwa hiyo, hakuna kazi nai-miss kama ya ubunge.

“Natamani niende ofisini kwangu, nikajiandae nikasome ili nikizungumza bungeni, Watanzania wasikie, hiyo ndiyo kazi ninayoipenda.

“Kwahiyo, kitendo cha kukaa miezi mitatu hospitalini nikiwa nimelala kitandani muda wote, mtu ukisema hii ni kutafuta kiki, nafikiri aidha hanifahamu au akili zake haziko sawa,” alisema Lissu.

 

KUHAMAHAMA WAPINZANI

Akizungumzia kitendo cha wanasiasa wa vyama vya upinzani kuhamia CCM, Lissu alisema hakiwezi kuua upinzani.

Alitolea mfano wa viongozi waliowahi kuwa Chadema kama vile Dk. Walid Amani Kabourou (Mbunge wa zamani Kigoma Mjini), Said Amour Arfi (Mbunge wa Mpanda Kati), Dk. Wilbrod Slaa (Katibu Mkuu Chadema), Patrobas Katambi (Mwenyekiti Bavicha na David Kafulila kuwa walihama na kujiunga CCM, lakini bado chama hicho kipo imara.

“Watu kwa sababu mbalimbali, aidha hawajui, wanasahau au wanajisahaulisha na historia yetu ya vyama vingi.

“Ukianza kuwafuatilia akina Kabourou, Arfi na Dk. Slaa ambao baada ya safari kuwa ndefu mno wakashukia njiani je, Chadema imekufa?

“Kafulila aliyekuwa NCCR-Mageuzi na juzi alikuwa Chadema na leo yuko CCM, hiyo itaua Chadema au Masha, Katambi?” alihoji Lissu.

 

MAMA SAMIA, MWINYI

Akiwazungumzia Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, alisema alipata faraja baada ya kumtembelea hospitalini.

“Ukiwa mgonjwa, hakuna kitu kizuri chenye faraja kama kupata mtu wa kuja kukujulia hali. Mzee Mwinyi aliniambia Mungu mkubwa, nitapona, nilishukuru sana,” alisema.

Mwisho.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles