25.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Profesa Mbilinyi ampa mbinu Rais Magufuli

MbilinyiNa Waandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa zamani wa Fedha, Profesa Mbilinyi, amesema ili Serikali ya Rais Dk. John Magufuli iweze kufanikiwa, inapaswa kuwa makini kuhakikisha inasimamia bajeti.

Pamoja na hali hiyo, amemtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kuhakikisha anasimamia bajeti ya Serikali aliyoiwasilisha bungeni na asikubali kumsikiliza mtu kwa kisingizio cha kuongeza matumizi ambayo hayakupangwa.

Profesa Mbilinyi aliyekuwa katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, alitoa kauli hiyo wiki hii, wakati akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu ofisini kwake Dar es Salaam.

Alisema ni vema wazingatie matumizi yanayokwenda sambamba na bajeti.

“Waziri azingatie ‘Expenditure’ ya Serikali kwa sababu ni hatari… awe makini kusimamia, hasa ile bajeti aliyowasilisha bungeni, ahakikishe wanakaa ndani ya makubaliano, asikubali kuongeza maana mwisho atajikuta hana tena bajeti wala mapato zaidi ya makaratasi pekee,” alisema.

 

UCHUMI WA GESI

Profesa Mbilinyi alisema Serikali itapata fedha nyingi katika sekta ya gesi, lakini umakini wa hali ya juu unahitajika katika kubana matumizi kulingana na jinsi itakavyokuwa inapata mapato.

“Wazingatie suala la matumizi ya Serikali kwa kuzingatia bajeti ileile iliyowasilishwa bungeni, hata kama mapato ya mafuta na gesi yakiongezeka wasiyatumie ovyo ovyo, nchi itazidi kuwa na shida siku zijazo wakati huo mafuta yakiwa yamekwisha,” alisema.

 

VIWANDA

Profesa Mbilinyi alisema iwapo sekta ya viwanda itasimamiwa kwa ufanisi, itasaidia kuzalisha fursa nyingi za ajira na kupunguza idadi ya vijana wasiokuwa na ajira mitaani.

“Tuna vijana wengi ambao wanahitumu elimu kwenye vyuo mbalimbali, kama unavyojua wasomi wetu wanaona tabu kwenda kujishughulisha na kilimo cha jembe la mkono. Kwa mfano, hawa ni nguvu kazi yetu ya kutosha, kukiwa na viwanda watakwenda kuzalisha huko viwandani na hatimaye tutaongeza mapato yetu,” alisema.

 

ELIMU BURE

Akizungumzia juu ya sera ya elimu bure aliyoitangaza Rais Magufuli kuwa Serikali itagharamia wanafunzi wa ngazi ya msingi na upili (sekondari) ili wote wapate elimu, Profesa Mbilinyi alisema inapaswa kusimamiwa kwa dhati kwa sababu elimu ni gharama.

“Rais Magufuli ameahidi Serikali yake itatoa elimu bure, anapaswa kusimamia kwa dhati ili kuhakikisha anaitimiza ndoto yake. Elimu ni gharama na kwa kuwa ameahidi lazima alipe, anaweza kufanikiwa kwa sababu naona amejidhatiti kwenye ukusanyaji wa mapato,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles