25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Profesa Lipumba, Lissu kukaa jukwaa moja?

lissu-na-lipumba

Na JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM

CHAMA cha ACT Wazalendo kinatarajia kuwakutanisha katika jukwaa moja Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.

Wanasiasa hao wanatarajiwa kukutana katika Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia ulioandaliwa na chama hicho Oktoba 8 mwaka huu.

Taarifa ya wanasiasa hao kukutana katika jukwaa hilo zilitolewa juzi na Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, alipozungumza na viongozi na wanachama wa mkoa wa Dar es Salaam ikiwa ni maandalizi ya mkutano huo.

CUF, NCCR Mageuzi na Chadema viliunganisha nguvu ya pamoja kuanzia kwenye Bunge Maalumu la Katiba kwa kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa wanasiasa hao kukutana ana kwa ana tangu Profesa Lipumba ajipojiuzulu uenyekiti wa CUF kutokana na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kukaribishwa katika umoja huo na kupewa nafasi ya kugombea urais.

Zitto alisema licha ya chama hicho kualika viongozi wakuu wa vyama vyote vya siasa nchini, lakini kimewaandikia barua binafsi wanasiasa hao ili washiriki kutoa mada kuhusu masuala ya Katiba na uchumi.

“Agenda ya kwanza katika mkutano wetu huo ni ya  Katiba kwa sababu mchakato wa Katiba mpya umekwama na hatujui tunaelekea wapi, tumemwandikia rasmi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aje kwenye mkutano wetu atuelezee, kama mjuavyo ni  mtaalamu wa katiba na mwanasheria, hatutamwita kama mwanaChadema” alisema Zitto na kuongeza:

“Halafu sasa hivi kuna mjadala mkubwa nchini juu ya  mdororo wa uchumi, watu hawana hela mifukoni, hivyo tumemwalika mchumi mbobevu Profesa Ibrahim Lipumba aje atuelezee tunatokaje katika hali hii na wote tumeshawaandikia barua za mialiko tunasubiri uthibitisho wao, chama chetu kinaangalia maslahi ya nchi hatujali mipaka ya vyama,” alisema.

Aidha kiongozi huyo wa ACT Wazalendo alisema lengo la kongamano hilo la kisiasa ni kutanua daraja la majadilano kuelekea 2020, huku kukiwa na mipango thabiti ya  kukiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Mkutano mkuu wa wanachama utakuwa ndiyo jukwaa la wanachama wote kuhoji utendaji na sisi ndiyo chama pekee chenye kufanya hivyo pia itakuwa ni sehemu ya kiongozi wa chama kutoa mwelekeo wa chama,” alisema Zitto.

Mbali ya wanasiasa hao pia wamealikwa wanasiasa kutoka nje ya nchi, akiwemo Samia Nkuruma, ambaye ni mgombea urais nchini Ghana atakayetoa mada juu ya nafasi ya mwanamke katika siasa za Afrika.

Wengine kutoka nje ya nchi wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo ni pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa ODM, Ababu Namwamba, ambaye kwa sasa  ni kiongozi wa Chama cha Labour cha nchini Kenya na atajadili changamoto za  vijana na wanamapinduzi katika siasa za vyama vyao.

Zitto aliongeza kuwa mgeni mwingine kutoka nje atakayepata nafasi ya kutoa mada katika mkutano huo ni aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha UPND cha Zambia, Hakainde Hichilema.

Alisema Hichilema atazungumzia siasa za upinzani na namna viongozi wa vyama hivyo wanavyoibiwa kura katika uchaguzi.

Aahidi mikutano misibani

Akizungumzia zuio la serikali katika kufanya mikutano ya hadhara, Zitto alisema wanasiasa hawawezi kukaa kimya bila kufanya siasa na kwamba ni lazima kubadilisha mbinu zitakazokuwa na manufaa kwa ajili ya kukabiliana na uminywaji wa demokrasia nchini.

“Katika wakati huu ambapo mikutano ya hadhara imezuiwa tunahitaji kufanya siasa na tutafanya hata katika misiba na maharusini lakini ni lazima kwanza tuwajenge watu wetu waelewe kuwa kuna ACT na malengo yake ni nini,”alisema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles