Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohammed Janabi amedai mfanyabiashara Yusuf Manji aliwahi kufanyiwa uchunguzi katika taasisi hiyo kuangalia kama vyuma vilivyopo katika moyo vimeziba ama la.
Profesa Janabi medai hayo wakati akitoa ushahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo Agosti 30, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha akiongozwa na mmoja wa mawakili wa Manji, Hajra Mungula ambapo anakuwa shahidi wa kwanza kumtetea Manji anayekabiliwa na mashtaka ya kutumia dawa za kulevya ikiwamo heroin.
Profesa Janabi amedai Manji aliwahi kulazwa katika taasisi hiyo mara mbili tofauti, Februari na Julai mwaka huu ambapo alipofika Februari alitokea Polisi akiwa na matatizo ya moyo na alikuwa akisikia maumivu upande wa kushoto wa moyo hivyo alifanyiwa uchunguzi kuangalia kama vyuma vilivyopo katika moyo wake vimeziba ama la.
“Alipofikishwa kwa matibabu alipewa dawa aina tatu tofauti za moyo na kabla ya hapo alikuwa na tatizo la mgongo na kukosa usingizi, kwa tatizo hilo alikuwa akipatiwa matibabu Hospitali ya Agha Khan,” amedai Profesa Janabi.
Shahidi amedai mgonjwa wa moyo mwenye chuma katika moyo wake, kabla hajawekewa chuma hicho huelezwa vitu ambavyo hatakiwi kutumia ikiwemo kuvuta sigara na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo heroine kwani yana athari kubwa na hufanya mirija kuziba na kusababisha kufanyiwa upasuaji mkubwa.
Wakili wa Serikali Mkuu, Timony Vitalis alipomuhoji shahidi huyo kama anajua athari za mgonjwa wa moyo kutumia dawa za kulevya, alijibu yeye ni daktari wa moyo na anazijua athari. Kesi hiyo itaendelea leo kwa mashahidi upande wa mshtakiwa kuendelea kutoa ushahidi.