Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umetakiwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili iwasaidie kutatua migogoro wanapokwama katika mambo ya sheria.
Wito huo umetolewa leo Januari 25,2023 na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel alipotembelea Banda la Brela katika maonyesho ya Wiki ya Sheria yanafanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma kuanzia Januari 24 hadi 30.
Prof. Ole Gabriel amesema uwepo wa migogoro inavunja moyo kwenye utendaji wa kazi na kwamba majukwaa kama hayo yanasaidia kujenga uelewa mpana kwa wananchi.
“Brela mnafanya kazi nzuri sana na maonyesho kama haya ni muhimu katika kuwajengea uelewa wananchi, hivyo yatumieni kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi ili iwasaidie kujenga uelewa wanapokuwa wamekwama katika mambo ya sheria.
“Kwani Watanzania wengi wanachangamoto ya uelewa wa mambo yanayohusu sheria, hivyo Brela endeleeni kuwasaidia wananchi kutatua shida za migogoro ili Taifa letu liweze kupiga hatua,” amesema Prof. Ole Gabriel.
Brela ni moja ya taasisi za Serikali zinazoshiriki maonyesho hayo yenye kauli mbiu ya “Nafasi ya Mahakama na Wadau katika kuboresha Mfumo wa Jumhishi wa Haki Jinai” ambapo imeendela kuyatumia kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi ikiwamo elimu, usajili wa majina ya biashara, kampuni na huduma nyingine.