25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Prof. Ndalichako: Serikali kuhakikisha afya, usalama wa wafanyakazi nchini 

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, amesema serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba afya na usalama wa wafanyakazi katika maeneo yote ya kazi nchini vinazingatiwa ili kuepuka ajali, magonjwa, vifo pamoja na uharibifu wa mali.  

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akitoa neno la shukrani kwa niaba ya menejimenti ya OSHA kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana, Ajira na Wenye ulemavu),  Prof. Joyce Ndalichako, wakati wa ziara yake katika ofisi ya OSHA Makao Makuu jijini Dar es Salaam.

Amesema hayo Februari 25, 2022 alipofanya ziara katika Ofisi za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) Dar es Salaam kwa lengo la kuona jinsi Taasisi hiyo iliyopo chini ya Wizara yake inavyotekeleza majukumu yake ikiwa ni takribani mwezi mmoja na nusu toka alipoteuliwa kuiongoza Wizara hiyo inayohusika na Masuala ya Kazi na Ajira.

“Sio lengo la serikali kuona watumishi wanapata madhara mahali pa kazi. Lengo ni kuzuia na ndio maana kuna hii Taasisi kwa ajili ya kushughulikia masuala ya usalama na afya mahali pa kazi ili kuhakikisha kwamba inatoa elimu, inafanya ukaguzi mahali pa kazi na kuhakikisha kwamba tahadhari zote zinachukuliwa ili kuzuia magonjwa na ajali na hivyo kuipunguzia mzigo serikali wa kuwahudumia watu wanaopata madhara mahali pa kazi,” alieleza Prof. Ndalichako.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na viongozi wa OSHA alipofanya ziara katika ofisi za OSHA Dar es Salaam kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa majukumu ikiwemo usimamizi wa sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 mbapo Taasisi ya OSHA inajukumu la kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo.

Aidha, amewaomba wafanyakazi wa OSHA kumpa ushirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo pamoja na kuwataka kufanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu na hivyo kuwawezesha Watanzania wote kufanya kazi katika mazingira salama ili kuongeza tija katika uzalishaji.

“Kimsingi nyinyi mnasimamia sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 ambapo sote tunafahamu kuwa pasipo afya njema hakuna mtu anayeweza kufanya kazi, afya ndio mtaji wa kila mtu lakini pia usalama mahali pa kazi kwani kama mazingira ya kazi sio mazuri hakuwezi kuwa na ufanisi.

“Hivyo, tunaitegemea sana Taasisi ya OSHA kuisaidia serikali kuhakikisha kwamba mazingira ya kazi yanakuwa salama na afya za wafanyakazi zinakuwa imara,” amesema Waziri Prof. Ndalichako.

Akizungumzia ziara hiyo ya Waziri mwenye dhamana ya Masuala ya Kazi, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema imekuwa na manufaa makubwa kwani pamoja kumwezesha Waziri kuifahamu Taasisi ya OSHA, imekuwa ni fursa kwa menejimenti na watumishi wa OSHA kuwasilisha baadhi ya changamoto zao ambazo zimepatiwa majibu na Waziri mwenye dhamana.

“Leo tumebahatika kutembelewa na Waziri wetu. Prof. Ndalichako ambaye kimsingi ametoka sekta nyingine na hivi karibuni ameteuliwa kuongoza Wizara yetu ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

“Hivyo, alikuja kuona namna gani tunatekeleza majukumu yetu ambapo tumepata fursa ya kumpitisha katika Sheria ya Usalama na Afya mahali pa kazi pamoja na taarifa ya utendaji wetu kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Vile vile tulipata fursa ya kumweleza baadhi ya changamoto zetu ambazo tunaamina kwamba atatusaidia kuzitafutia ufumbuzi,” amesema Mwenda.

Watumishi wa OSHA wakiwa katika kikao kifupi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, (hayupo pichani) alipofanya ziara katika Ofisi za OSHA Dar es Salaam kwa lengo la kuangalia utekelezaji majukumu ya Taasisi hiyo.

Katika ziara hiyo ambayo ni mwendelezo wa ziara katika Taasisi mbali mbali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Waziri Ndalichako alielezwa majukumu ya msingi ya OSHA pamoja na taarifa ya utekelezaji majukumu hayo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles