27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Upanga Mashariki wadhamiria kupambana na Uviko – 19

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Shule za msingi na sekondari zilizoko katika Kata ya Upanga zimepatiwa vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa Uviko – 19 ili kupunguza maambukizi na kuhakikisha wanakuwa salama.

Vifaa hivyo vinavyojumuisha vitakasa mikono, sabuni, ndoo za maji tiririka na vipeperushi vimetolewa kwa Shule za Msingi Diamond, Maktaba, Upanga, Olympio, Zanaki pamoja na Shule ya Sekondari Zanaki.

Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Saad Khimj, akimkabidhi vifaa vya kujikinga ugonjwa wa Uviko Msimamizi wa usafiri kwa wanafunzi wanaosoma shule zilizoko Kata ya Upanga Mashariki, Twaha Lusama.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Saad Khimj, amesema suala la Uviko ni ajenda ya dunia kwani ugonjwa huo bado upo na unaendelea kugharimu maisha ya watu.

“Niwapongeze watu wa Upanga Mashariki mmesimama na ajenda ya mheshimiwa rais na kujali afya za wananchi, tuendelee kupambana kuhakikisha wananchi wanaendelea kubaki salama,” amesema Khimj.

Aidha amesema jiji hilo limepewa miradi mingi ya kupambana na ugonjwa huo ikiwemo ujenzi wa madarasa 255 yenye thamani ya Sh bilioni 5.1 na vituo vitatu vya afya vinavyojengwa Kata za Mchikichini, Segerea na Kipunguni.

Khimj pia amewataka wananchi kulinda heshima iliyopata Jiji la Dar es Salaam kwa kufanya vizuri katika usafi kwani itaongeza watalii nchini.

Naye Diwani wa Kata ya Upanga Mashariki, Sultan Ahmed Salim, amesema msaada huo umetolewa kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali na viongozi wa serikali za mitaa na kata na kwamba licha ya watoto kutougua lakini wanaweza kubeba virusi vya ugonjwa huo na kuvipeleka kwa wazazi wao au watu wengine wanaoishi nao nyumbani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kibasila, Rukia Ryami, amesema walishawishi wakazi wa maeneo hayo kupata chanjo na kuwasihi waendelee kujikinga kwani ugonjwa bado upo.

Ofisa Elimu Kata ya Upanga Mashariki, Dorah Lusanda, ameshukuru kwa msaada huo na kusema wana wanafunzi wengi kutoka sehemu mbalimbali hivyo utasaidia kupunguza maambukizi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles