Na CHARLES MULLINDA-DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema ripoti ya uchunguzi wa Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) dhidi ya tuhuma za ufisadi zinazowakabili wakurugenzi watano wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) itawatoa jasho.
Amesema ripoti hiyo itathibitisha pasipo kuacha wingu la shaka iwapo wakurugenzi hao ni malaika, wachapakazi, wanalipenda taifa au vinginevyo.
Prof. Muhongo aliyasema hayo katika mahojino na Gazeti la MTANZANIA lililotaka kujua mwenendo wa uchunguzi wa tume inayochunguza tuhuma za ukiukwaji wa sheria na kanuni za ununuzi wa umma, na ukiukukwaji wa sheria na kanuni za utumishi wa umma hususan mgongano wa maslahi.
Nyingine ni kubadili matumizi ya fedha za bajeti bila idhini ya mamlaka za juu na kutotolewa taarifa muhimu, nyeti na hasa kuhusu shughuli za shirika.
Wakurugenzi waliosimamishwa kazi kupisha uchunguzi ni Mkurugenzi Mkuu, Dk. James Mataragio, Mkurugenzi wa Fedha, George Seni, Mkurugenzi wa Mkondo wa Juu, Kelvin Komba, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani, Gabriel Mwero na Mkurugenzi wa MPMU, Edwin Riwa.
Katika majibu yake kwa MTANZANIA, Prof. Muhongo ambaye alikataa kulizungumzia jambo hilo kwa undani akisema hakuhusika kuiunda tume hiyo, alisema baada ya wakurugenzi waliotuhumiwa kusimamishwa, Takukuru ilipiga kambi TPDC kufanya uchunguzi ambao ripoti yake itatoa jasho.
“Tume inayochunguza siyo ya waziri. Takukuru imeenda TPDC, hii ni serikali au mnataka tuongee mambo ya serikali?
“Kuna bodi ndiyo inayoamua, wanaokutuma kawaambie Takukutu imepewa kazi pale, nipeni taarifa za kweli.
“Takukuru ilipiga kambi hapo, kapate ripoti ya Takukuru utatoka jasho… wewe si unataka nikwambie ukweli…. Tume itasema ukweli, tulia,” alisema Prof. Muhongo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC, Profesa Sufiani Bukurura aliliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa mbichi na mbivu kuhusu tuhuma hizo zitawekwa wazi katika uchunguzi wa kina unaofanywa na tume.
Kabla ya wakurugenzi hao kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi, Gazeti la MTANZANIA lilikuwa la kwanza na pekee lililoripoti kuhusu mradi wa utafiti wa mafuta na gesi wa TPDC katika maeneo ya Kaskazini na Magharibi mwa Ziwa Tanganyika, Songosongo, Mandawa na Eyasi–Wembere, kuwa utekelezaji wake ulighubikwa na mchezo mchafu.
Gazeti hili pia ndilo lililoripoti taarifa kuwa Hazina ilikataa kulipa mishahara na posho za maofisa 14 wa juu wa TDPC kwa sababu ya kukiukwa taratibu za ajira zao.