Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amepokea taarifa ya utekelezaji wa agizo alilotoa la kuundwa katiba mpya ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (MBOMIPA).
Pia ameagiza kufanyike kwa marekebisho ya mwisho kabla ya kuwasilishwa kwa wananchi kwa ajili ya mijadala.
Waziri huyo alipokea taarifa hiyo juzi katika kikao alichokiitisha kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa baada ya kufanya ziara ya kazi kwenye eneo la jumuiya hiyo Kijiji cha Tungamalenga.
Alibaini upungufu mbalimbali wa katiba na kuamua kuagiza kuundwa upya katiba na kuvunja bodi ya wadhamini.
Miongoni mwa upungufu ambao ulibainika ni katiba iliyokuwapo awali kukinzana na sheria mama na kanuni zake.
“Baada ya michango yote hii mizuri tuliyotoa hapa leo, nendeni sasa mkairekebishe vizuri izingatie maeneo yote ya msingi ikiwamo mgawanyo sawa wa mapato, kuzingatiwa kwa maeneo ya mapito ya wanyamapori na idadi ya wanachama ijumuishe vijiji vyote vilivyoanzisha jumuiya hiyo kuepusha migogoro ya baadaye inayoweza kujitokeza,” aliagiza Profesa Maghembe.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume iliyoundwa na Waziri Maghembe kuchunguza mgogoro huo wa MBOMIPA.
Wengine ni baadhi ya wajumbe wa tume hiyo na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Iringa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Amina Masenza.
Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori MBOMIPA iliundwa mwaka 2007 ikiwa na wanachama ambao ni vijiji 21 vya tarafa ya Idodi za Pagawa kwenye halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijini mkoani Iringa.
Eneo la jumuiya hiyo lina ukubwa wa kilomita za mraba 777 na linapakana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.